Tuesday 3 September 2013

KWAHERI CHADEMA, KARIBU CCM DADAKE MBOWE:

DADA YAKE FREEMAN MBOWE ARUDISHA KADI YA CHADEMA,AJIUNGA CCM NA KUKABIDHIWA KADI YA UANACHAMA


Picture: Grace Mbowe
DADA wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Grace Mbowe, amejiunga na Chama Cha Mapinduzi ( CCM) akitokea Chadema, kwa kile alichodai haoni jambo jipya katika chama hicho.

Grace amesema amehama kutokana na kuwepo propaganda zisizotekelezeka. Hata hivyo, amesisitiza kwamba kuwepo kwake katika Chadema, siyo kwa sababu ya familia.

Alikabidhi kadi hiyo jana kwenye ofisi za CCM Wilaya ya Hai. Alisema itikadi za kisiasa, zisihusishe masuala ya kifamilia, kwani upendo wao uko pale pale.

Alisema kilichomfanya kujiunga na chama hicho ni utashi wake. Alidai CHADEMA wanafanya propaganda za 
kuwadanganya wananchi.

Alisema itikadi za chama, haziwezi kuingilia masuala ya kifamilia, hivyo kwake siyo ajabu kuondoka CHADEMA, kwani kila mtu ana utashi wake wa kisiasa.

“Nimeamua kwa hiari yangu mwenyewe bila kushawishiwa na mtu, ndio maana nimetoka Dar es Salaam kuja Hai kwa ajili ya kurejesha kadi ya CHADEMA na kujiunga na CCM, suala la itikadi lisihusishe masuala ya kifamilia kwani upendo wetu upo palepale,”alisema Mbowe.

Alisema, “kuwapo kwangu CHADEMA siyo kwa sababu ya familia, hivyo hakuna wa kunizuia, natoka kwa utashi wangu, na tutaendelea kuheshimiana na mdogo wangu Freeman Mbowe katika masuala ya kifamilia.”

“Freeman Mbowe ni mdogo wangu wa kuzaliwa kabisa, hakunishawishi kuingia CHADEMA, hivyo sioni haja ya kuendelea kubaki huku wakati sioni jambo jipya, mimi tangu naifahamu CCM iko vile vile, bali propaganda za upinzani ndizo zinawalaghai wananchi,” alisema.
Picture: Grace Mbowe, Hassan Mtenga
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro, Hassan Mtenga kushoto akimkabidhi yadi ya CCM, Grace Mbowe, baada ya kutoka CHADEMA kwa kile alichodai hakuna jambo jipya.
Aliviasa vyama vya siasa, kuwa sasa umefika wakati wa kuacha malumbano na maandamano ya itikadi, yasiyokuwa na faida yoyote, badala yake huu ni muda wa kujenga nchi kwa ushirikiano.

Awali, akipokea kadi ya CHADEMA, Katibu wa CCM Wilaya ya Hai, Hassan Mtenga alisema alichokifanya Grace ni uamuzi wa busara, baada ya kutazama Chadema ilipo na inapokwenda.

Alisema wimbi la wanachama wa Chadema kurudisha kadi na kujiunga na CCM, limekuwa kubwa wilayani Hai. Alisema tangu Januari hadi sasa amepokea wanachama 530.

Mtenga aliwataka wananchi kutambua kwamba Jimbo la Hai, siyo kitovu cha upinzani bali CHADEMA ni chama kilichotoa upinzani kwa CCM katika uchaguzi mkuu wa 2010. Alisema hali hiyo, ilitokana na makundi ya CCM.Alisema kwa sasa watu asitarajie tena suala hilo kutokea.

 Source HabariLeo