Tuesday, 6 August 2013

Mamia ya wahamiaji haramu kutoka nchini Rwanda wakiwa na ng’ombe zaidi 900 wameanza kuondoka nchini kurejea kwao kutokana na agizo la Rais Jakaya Kikwete kuwataka waondoke Tanzania kabla ya siku 14. 
 
Aidha, imeelezwa kuwa kumekuwapo ongezeko la askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mkoani Kagera hasa wilayani Ngara hali inayozua hofu kwa baadhi ya wananchi, huku ikiongeza msukumo kwa wahamiaji haramu kuondoka.
 
Akiwa katika ziara mkoani Kagera, Rais Kikwete alitoa agizo la kuwataka wote waliokuwa wakiishi nchini kinyume cha sheria waondoke mapema jambo lililotakiwa kuanza kutekelezwa Julai 29 na kukamilika Agosti 10 mwaka huu.
 
Alisema kuwa wahamiaji haramu na wale wanaoendesha ama kuhusika na ujambazi, uhamiaji haramu na uingizaji haramu wa mifugo waamue kuchukua hatua mwafaka za kuondoka mapema kabla vyombo vya ulinzi na usalama kuanza operesheni maalumu ya kuwasaka.
 
Tayari idadi kubwa ya wafugaji wenye makundi ya ng’ombe imeanza kuondoka kuelekea eneo la mpakani la Rusumo kutoka ardhi ya Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa agizo hilo la Rais Kikwete.
 
Akizungumza na Mwananchi Jumapili kwa njia ya simu, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Costantine Kanyasu alisema kwamba idadi kubwa ya wafugaji waliokuwa wakiishi kinyume cha sheria, imeitikia wito wa agizo la Rais na kuanza kuondoka kwa hiyari yao.
 
Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na idadi kubwa ya wahamiaji kuanza kuondoka, bado wapo ambao hawajaondoka kutokana na kudai kuwa na vibali walivyovipata kutoka Ofisi ya Uhamiaji na kubainisha kwamba vibali hivyo vitakaguliwa kwa umakini wakati wa operesheni maalumu ili kujua uhalali wake.
 
“Jambo hili la wahamiaji haramu lilikuwa kero kubwa, siyo tu kwa Wilaya ya Ngara, bali mkoa mzima wa Kagera, lakini tunashukuru sasa wameanza kuondoka, wamebaki hao wenye vibali. Ni lazima vibali hivyo tutavikagua maana vipo vilivyotolewa kinamna,” alieleza Kanyasu.
 
Alionya kwamba jukumu la kuwaondoa kwa nguvu wahamiaji haramu pamoja na wafugaji linasubiri muda wa mwisho ili kuanza kutekelezwa kama Rais Kikwete alivyoagiza.
 
Hofu ya Wanajeshi kuongezeka

Akizungumzia suala la wanajeshi kudaiwa kuongezeka wilayani Ngara, Kanyasu alisema kwamba katika wilaya yake kuna kikosi cha dharura kinachokaa katika moja ya kambi za JWTZ kikikuwa na idadi kubwa ya askari lakini wananchi hawakuwa na taarifa nacho ila kutokana na sababu za kiusalama.
 
“Unajua kuna kelele za hapa na pale na haya majibizano yanayotokea baina ya Rwanda na Tanzania. Haya ni kama yamewastua watu na kudhani kuwa askari wetu wa Kikosi cha Dharura waliopo hapa Ngara wameletwa maalumu kutokana na tahadhari,” alisema na kufafanua kuwa askari hao wapo siku zote kwa ajili ya kulinda mipaka ya Tanzania. 
 
Hata hivyo, mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kutulia na kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo.

Rais Kikwete aliagiza operesheni hiyo ya kuwaondoa wahamiaji haramu ifanyike katika Mikoa ya Kigoma, Kagera na Geita kwa wakati mmoja ikisimamiwa na vyombo vya ulinzi na usalama yaani JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa na Uhamiaji akiwaonya wahalifu kuwa hapatakuwa na mahali pa kukimbilia wala kujificha.