Friday, 10 May 2013


       CHAMA CHA MAPINDUZI.
                                   TAWI LA UNITED KINGDOM.
Website: www.ccmuk.org, ccmuk.org/blog, Facebook – chama cha mapinduzi uingereza, Twitter CCM UK.
       
CCM UK INAUNGANA NA WATANZANIA WOTE  KUPINGA VIKALI KITENDO CHA KIGAIDI KILICHOTOKANA NA ULIPUAJI WA BOMU KANISA KATOLIKI LA OLASITI JIJINI ARUSHA.
Uongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi Tawi la Uingereza  tunapenda kuungana na Watanzania wote wapenda amani katika kuwapa salamu zetu za pole  Viongozi na Waumini wa Kanisa Katoliki la Olasiti jijini Arusha , kutokana na tendo shambulizi la kigaidi la kutupwa bomu kanisani hapo lililosababisha Watanzania Wawili kupoteza maisha na zaida ya 60 kujeruhiwa.
CCM UK siku zote inawausia Watanzania kulinda Amani yetu na kushikamana kwa pamoja wakati wa kufanya hivyo bila ya kujali tofauti zetu za kiitikadi , kabila , rangi wala siasa .
CCM UK tunapenda kutoa shukrani za pekee kwa Mwenyekiti wetu wa Taifa na Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuongoza kwa mfano bora pale alipokatiza Ziara ya muhimu nchini Kuwait na kurudi Nyumbani kwa haraka ili awe pamoja na Wananchi wake katika kuomboleza na kukemea vikali shambulio hilo lililofanywa na mtu au watu katili, waovu na wenye dhamira mbaya na nia mbaya kwa Tanzania na watu wake.
Aidha CCM UK  inaishukuru Serikali na Vyombo Vya Dola kwa hatua za haraka zilizochukuliwa katika kutafuta wahusika wa tukio hili la kinyama na lisilo na msingi na kuwaomba watanzania kuwa  watulivu wakati huu na kuviachia vyombo vya dola kufanya kazi yake na kuchukua tahadhari juu ya watu waovu wanaotaka kuwavuruga na kuwafarakanisha kwa misingi ya dini.
CCM UK inatoa salamu za pole na kuwafariji  familia za wale wote waliopoteza Maisha yao na kuwaombea majeruhi wote  walioumia katika tukio hili wapate nafuu ya haraka na waendelee na shughuli zao za ujenzi wa taifa.
                                                               
Imetolewa na Idara ya Itikadi, Siasa na Uenezi
CCM - UNITED KINGDOM.