Sunday, 3 August 2008

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA,MHESHIMIWA JAKAYA
MRISHO KIKWETE,KWA WANANCHI,
TAREHE 31 JULAI,2008..
---
Ndugu Wananchi;Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima na kuniwezesha kuzungumza nanyi leo mwishoni mwa mwezi wa Julai,2008.Nasikitika na nawataka radhi kwamba kwa miezi ya Aprili,Mei na Juni,sikuweza kupata fursa ya kuzungumza nanyi kupitia utaratibu wetu huu mzuri.
Sababu kubwa iliyonifanya nishindwe kuzungumza na Taifa, ni ule ukweli kwamba, tarehe za mwisho wa mwezi katika miezi hiyo zilinikuta nikiwa nje ya nchi kikazi. Safari ambazo nisingeweza kuacha kwenda labda ningekuwa nimepata dharura kubwa.
Huko nyuma katika mazingira ya namna hii nilitumia utaratibu wa kurekodi hotuba yangu kabla ya kuondoka na kuacha itangazwe siku ya mwisho wa mwezi ilipofikia. Utaratibu huo ulikidhi haja, lakini nikaambiwa kuwa haukufurahiwa sana na wengi hasa pale ilipotokea kuwa Rais wao waliyemsikia redioni leo akihutubia,walimsikia jana akiwa nchi ya mbali na wanajua hajarejea.Kwa sababu hiyo basi,nikaona kwamba nizungumze katika utaratibu huu wa mwisho wa mwezi pale tu nitakapokuwa ndani ya nchi.
Hata hivyo, uamuzi huo umezua manung’uniko yake hasa pale ambapo miezi mitatu mfululizo imetokea Rais kutozungumza kwa sababu ya kuwa nje ya nchi kikazi.Maoni ya pande zote nimeyasikia,nipeni muda nitafakari lipi bora tufanye.Ndugu Wananchi;
Ni makusudio yangu leo kuelezea matokeo ya safari zangu hizo.Mwishoni mwa mwezi wa Aprili nilikwenda Ethiopia na Uganda.Kule Addis Ababa,Ethiopia tarehe 28 Aprili,2008 nilitimiza jukumu la kushuhudia makabidhiano ya ofisi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika baina ya Mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa uongozi, Mheshimiwa Prof.Alpha Oumar Konare,na Mwenyekiti mpya Mheshimiwa Jean Ping.
Ni utaratibu uliowekwa kuwa shughuli hiyo ya makabidhiano ya ofisi husimamiwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika wa wakati huo.Nilitumia nafasi hiyo kuzungumza na uongozi mpya wa Kamisheni ya Afrika juu ya matarajio yangu na viongozi wenzangu wa Afrika kwao. Aidha,nilizungumza na wafanyakazi wa Umoja wa Afrika pamoja na kuwatambulisha viongozi wapya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika kwao.
Siku iliyofuata niliitumia kuzungumza na Wajumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kuhusu hali ya amani na usalama ya Bara letu.Tulitumia muda mwingi kujadili migogoro inayolikabili Bara letu na hatua muafaka za kuchukua kuitafutia ufumbuzi.Tarehe 30 na 31 Aprili,2008 nilikuwa Uganda kwa mazungumzo na Rais Yoweri Museveni wa nchi hiyo.
Pamoja na kuzungumzia masuala yahusuyo nchi zetu za Afrika Mashariki na Afrika tulijadili hali ya usalama na amani ya eneo la Maziwa Makuu.Hususan tulizungumzia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Burundi. Matokeo ya mazungumzo yetu hayo ni mambo mawili muhimu.
Kwanza, ni mkutano uliofanyika Dar es Salaam kati ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo tarehe 11 Mei,2008.Katika mkutano huo nchi hizo mbili jirani zilifanikiwa kuzungumzia tofauti zao na kuafikiana kuhusu namna ya kuzimaliza.
Pili,kuhusu Burundi ni kufanikiwa kumrejesha Burundi Bwana Agathon Rwasa, Kiongozi wa PALIPEHUTU-FNL na viongozi wenzake waandamizi wa chama hicho. Kitendo hicho kimefunga ukurasa wa shughuli za usuluhishi wa mgogoro wa Burundi zilizotuchukua takriban miaka 13 (tangu Disemba, 2005).
Aidha, kitendo hicho sasa kimefungua njia ya kumaliza tatizo la wakimbizi wa Burundi. Wapo waliokuwa wanasita kurejea kwako kwa sababu ya viongozi kuwa nje ya Burundi. Sasa wingu hilo limeondoka. Ni matumaini yangu kuwa kasi ya wakimbizi hao kurudi kwao itaongezeka.
Ndugu Wananchi;
Mwishoni mwa mwezi Mei, 2008 nilikuwa nchini Japan kuongoza ujumbe wa viongozi wa Afrika katika Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Tokyo Kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD IV) uliofanyika Yokohama kuanzia tarehe 27 hadi 30 Mei, 2008.
Ujumbe wa Afrika niliouongoza nikiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, ulikuwa na Wakuu wa Nchi na Serikali wapatao 40.Huu ulikuwa ni moja ya mikusanyiko mikubwa ya viongozi wa Afrika kwa mikutano nje ya Afrika.
Ndugu Wananchi; Mikutano ya TICAD ilianza mwaka 1993 na hufanyika kila baada ya miaka 5. Wazo la kuwa na mikutano hii liliasisiwa na Mheshimiwa Morihiro Hosokawa, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan wakati ule.Madhumuni ya Mikutano hii ni kusaidia kuongeza kasi ya maendeleo ya Bara la Afrika.
Serikali ya Japan iliamua kutumia mikutano hii kuchangia nguvu zake za kiuchumi na kiteknolojia na zile za nchi rafiki zake pamoja na za mashirika ya kimataifa yanayojihusisha na masuala ya maendeleo kusaidia kukuza uchumi wa Afrika na kuboresha hali ya maisha ya watu wa Bara la Afrika. Katika mkutano uliopita wa TICAD, nchi 34 marafiki wa Japan na Afrika zilishiriki ikiwa ni pamoja na mashirika ya kimataifa 75.
Maamuzi mengi ya msingi yamefanywa na ahadi nyingi za manufaa kwa maendeleo ya nchi za Afrika na watu wake yalifanywa.Kama maamuzi hayo yaliyojumuishwa katika Tamko la Yokohama na Mpango wa Utekelezaji wa Mkutano wa Nne wa TICAD yatatekelezwa, itasaidia sana kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Afrika kwa kasi zaidi.
Ndugu Wananchi;
Miongoni mwa maamuzi muhimu yenye maslahi kwa Afrika ni haya yafuatayo:(a) Serikali ya Japan itaongeza mara mbili misaada ya maendeleo inayotoa kwa nchi za Afrika.(b) Maeneo ya kipaumbele kwa misaada ya Japan itakuwa ni kuendeleza miundombinu hususan barabara, bandari, reli, usafiri wa anga,maji na umeme.
(c) Japan itasaidia Afrika kuongeza mara mbili uzalishaji wa mpunga.(d) Japan kusaidia Afrika kuendeleza elimu na huduma ya afya.Kwa upande wa huduma ya afya, kipaumbele kimewekwa kwenye kupambana na UKIMWI na kupunguza vifo vya watoto na kina mama kwa matatizo ya uzazi.
(e) Japan kuongeza misaada kwa nchi za Afrika kukabili athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani au kwa neno la kitaalam tabia nchi; na(f) Kwa nia ya kukuza uwekezaji wa makampuni ya Kijapani Barani Afrika, serikali ya Japan imetenga dola 2.5 bilioni kwa ajili ya kusaidia wawekezaji wa nchi hiyo watakaowekeza Afrika.Ndugu Wananchi; Hayo ndiyo matokeo ya Mkutano wa Nne wa Tokyo kuhusu Afrika.Ni matokeo yenye matumaini makubwa kwa Afrika kwa maana mbili: Kwanza, tofauti na mikutano iliyopita, safari hii mfumo wa ufuatiliaji umetengenezwa (Follow up mechanism). Hii inatupa imani kuwa yale yaliyokubaliwa yatafuatiliwa kwa dhati.
Pili, kwa maana ya yale yaliyokubaliwa na kuamuliwa kuwa ni mambo yenye maslahi makubwa kwa nchi zetu na watu wake.
Hata hivyo,ndugu wananchi, mambo haya mazuri watayapata wale watakaoyachangamkia. Nchi zitakazopeleka mapendekezo yao ya miradi watanufaika, na wale ambao hawatafanya hivyo watakosa.Kwa kutambua ukweli huo nimeziagiza Wizara husika chini ya uongozi na uratibu wa Wizara ya Fedha na Uchumi watayarishe miradi na kuiwasilisha kwa Serikali ya Japan mapema iwezekanavyo.
Ndugu Wananchi; Wakati wa Mkutano wa TICAD tarehe 29 Mei,2008 kulifanyika mkutano maalum wa kuzungumzia tatizo la bei kubwa za chakula duniani.Nilipewa heshima ya kuwa Mwenyekiti wa mkutano huo ulioitishwa na Benki ya Dunia ikishirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO),Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo(IFAD)na Shirika la Dunia la Chakula (WFP).
Katika mkutano huo ilibainika kuwa bei za vyakula takriban katika nchi zote duniani imeongezeka mara mbili katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kwamba bei inatarajiwa kuendelea kupanda mwaka huu na hata mwaka ujao.Ilielezwa pia kwamba zipo sababu kadhaa zinazosababisha bei kupanda lakini kubwa zaidi ni:
(a) Chakula kilichopo kuwa kidogo kuliko mahitaji;
(b) Kupanda kwa gharama za uzalishaji kwa sababu ya kupanda sana kwa bei ya mafuta na bei ya mbolea;
(c) Mabadiliko ya hali ya hewa duniani kunakosababisha ukame na mafuriko ya mara kwa mara siku hizi; na
(d) Kupungua kwa kilimo cha nafaka kwa sababu ya kilimo cha mazao ya kuzalisha nishati.
Ndugu Wananchi; Kwa kauli moja mkutano umekubaliana kuwa kwa upande wa Afrika suala la msingi ni kuwasaidia wakulima wa Afrika waongeze tija kwenye kilimo.Hili likifanyika Afrika inao uwezo siyo tu wa kujilisha wenyewe bali pia wa kulisha watu wengi wengine duniani.Mkutano ulipongeza juhudi zinazoendelea kufanywa na mashirika hayo manne ya kimataifa kusaidia nchi za Afrika kuendeleza kilimo.
Aidha, wito ulitolewa kwa nchi zilizoendelea na mashirika ya fedha ya kimataifa kuunga mkono jitihada hizo zikiwemo zile za kuwawezesha wakulima wadogo wadogo kupata mbegu bora, mbolea na mikopo.
Nafurahi kwamba tangu mkutano ule kuna utambuzi mkubwa zaidi na vuguvugu la kuwasaidia wakulima wadogo wa Afrika limeongezeka. Na, sisi kiserikali tumeshaomba Tanzania ijumuishwe katika jitihada hizo.Tunasubiri majibu. Iwapo tutafanikiwa kujumishwa na kupatiwa misaada tuliyoomba, matatizo ya sasa ya upatikanaji wa mbegu, mbolea na mikopo kwa wakulima wadogo yatapungua.
Ndugu Wananchi; Nafurahi pia kwamba tarehe 7 Julai,2008 nchi yetu ilipewa heshima nyingine kubwa ya kuongoza ujumbe wa Marais saba wa Afrika kwenye Mkutano wa Mataifa Manane yenye Viwanda Vingi Duniani (G-8).Mataifa hayo hukutana kila mwaka kujadili hali ya uchumi wa dunia na mwelekeo wake.
Kwa mwaka huu wa 2008, nchi hizo zilikutana huko Hokkaido nchini Japan mwanzoni mwa mwezi huu.Mimi na viongozi wenzangu wa Algeria, Senegal,Ghana,Afrika Kusini,Nigeria na Ethiopia tulitumia fursa hiyo kuelezea matatizo yanayolikabili Bara la Afrika na kusisitiza haja ya wajibu wa nchi zilizoendelea zikiongozwa na Kundi la Nchi Nane zenye viwanda vingi duniani, kuzisaidia nchi za Afrika kuondokana na umaskini uliokithiri na kuwa nyuma kwa kimaendeleo. Tulisisitiza kama tulivyofanya katika mkutano wa Nne wa TICAD haja ya kuongeza misaada ya maendeleo kwa Afrika.
Tuliwakumbusha viongozi wa G-8 kuhusu ahadi yao walioitoa kwenye mkutano wao wa Gleneagles mwaka 2005 kuhusu kuongeza misaada ya maendeleo kwa Afrika. Tumewataka watekeleze.
Aidha, kuhusu vipaumbele,tulisisitiza umuhimu wa kuongeza misaada inayotolewa kuendeleza miundombinu barani Afrika, kwani maendeleo hayatawezekana bila barabara nzuri, bandari, usafiri wa anga,umeme,maji na mawasiliano.Tuliitumia nafasi hiyo kuwasilisha kilio chetu kuhusu matatizo ya kupanda sana kwa bei za chakula na mafuta ya petroli duniani na athari zake kwa watu wa nchi zinazoendelea za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.Tumeelezea kwa kina athari zake na hasa tishio la kufuta mafanikio kiasi yaliyopatikana na kurudisha nyuma jitihada za kujiletea maendeleo.
Tuliowaomba Wakubwa hao wafanye kila wawezalo kuzuia kupanda holela kwa bei za mafuta na kuzisaidia nchi maskini na zinazoendelea za Afrikakukabili athari za kupanda kwa bei ya mafuta na bei ya chakula. Kama tulivyosema kwenye Mkutano wa TICAD na katika mkutano wa G-8 nako tuliomba kwa upande wa tatizo la upungufu wa chakula,nguvu zielekezwe kwenye kusaidia nchi zetu kufanya mageuzi ya kilimo na siyo kwenye kupewa misaada ya chakula pekee. Ujumbe wetu ulipokelewa vizuri na kuahidiwa kusaidiwa.Tunachosubiri sasa ni kuona vitendo.
Tutaendelea kufuatilia na kukumbushia bila ya kuchoka.Ndugu Wananchi; Mwishoni mwa mwezi wa Sita sikuweza kuzungumza na taifa kwa sababu ya kwenda Misri kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika.Ulikuwa mkutano mgumu kwa kiasi chake, hasa kwa mie niliyekuwa Mwenyekiti.Hata hivyo,nilifurahi kuwa hatimaye mambo yaliisha vizuri hata kuliko tulivyotarajia.
Nilifurahi sana pale rai yangu ya kujipa muda wa kutosha wa kujadili masuala ya maendeleo ya Afrika ilipokubaliwa.Niliomba hivyo kwa sababu tumekuwa na mazoea ya kutumia muda mwingi kujadili masuala ya siasa na migogoro.Watu wan chi zetu hawakuishi kwa siasa pekee. Safari hii tulijipa muda wa kutosha kujadili masuala ya maendeleo ya Afrika. Kuendeleza rasilimali maji na utekelezaji wa malengo ya Milenia barani Afrika yalikuwa ndiyo mambo makubwa yaliyotuchukulia muda mwingi.Kwangu mimi kutoa nafasi stahiki kuzungumzia masuala ya maendeleo ya nchi zetu na watu wake ni hatua kubwa ya maendeleo kwa Umoja wa Afrika. Hili ni jambo la faraja sana na nimeeleza matumaini yangu kuwa utaratibu huu tutaudumisha na kuuendeleza.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa siasa na migogoro, mambo mawili yalichukua muda mwingi wa mjadala kwenye mkutano wetu. Mambo hayo ni:
(a) Uanzishaji wa Serikali ya Umoja wa Afrika.
(b) Mgogoro wa Zimbabwe. Nafurahi kwamba pamoja na ugumu wa mijadala lakini hatimaye tulielewana vizuri kuhusu nini cha kufanya. Kuhusu Serikali ya Umoja ya Afrika tumekubaliana kuhusu viashiria na vichocheo vya kuwezesha Serikali hiyo kuwepo. Hata hivyo, hatukuweza kuelewana kuhusu lini Serikali hiyo inaweza kuundwa na muundo wake. Bado kuna tofauti kubwa za mawazo miongoni mwetu. Tumekubaliana tuendelee kulizungumza suala hilo kikao kijacho.
Kuhusu Zimbabwe, tulikubaliana kuwa,pamoja na kasoro zilizojitokeza wakati wa mchakato wa uchaguzi na kutia dosari kwa uhalali wake,bado jawabu litapatikana kwa pande husika kukaa chini na kuzungumza.Nafurahi kwamba yale tuliyoamua yafanyike yameanza kutekelezwa. Mchakato huo umeanza.Tuwatakie kila la heri ndugu zetu wa Zimbabwe mazungumzo yakamilike salama na nchi yao irejee katika hali yake ya kawaida na wananchi wa nchi hiyo waanze kazi ngumu ya kujenga upya taifa lao.
Ndugu Wananchi; Katika kipindi cha miezi mitatu hii ambayo sikupata nafasi ya kuzungumza na taifa. Kumekuwepo na matukio kadhaa hapa nchini yaliyogusa maisha,nyoyo na hisia za watu kwa namna mbalimbali.Yalikuwepo mambo mazuri,yalikuwepo mambo magumu na hata ya huzuni na majonzi. Aidha,yalikuwepo mambo yaliyoleta mtikisiko kwa jamii na hata kwa taifa na utaifa wetu. Kwa vile mambo ni mengi kiasi sitapata nafasi ya kuyazungumzia yote moja baada ya jingine.Napenda kuitumia nafasi hii kuwatoa wasiwasi na kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa, taifa letu bado ni moja na watu wake bado ni wamoja.
Tofauti za mawazo na fikira miongoni mwetu hazitakosekana.Naomba tuyaone mawazo na fikira hizo kuwa changamoto za kushughulikia katika kuimarisha umoja wa taifa letu na mshikamano wa watu wake.Napenda kuwahakikishia kuwa sisi viongozi wenu tunayatambua hayo na tunayashughulikia. Hakuna kubwa la kutuzidi kimo na kwamba hakuna litakaloharibika. Kwa vile nia yetu ni njema na penye nia pana njia sina shaka mambo yatakuwa sawa.Nawaomba tuwe watulivu kwani utulivu wetu ni sehemu ya jawabu.Ni imani yangu kuwa kila anayeitakia mema nchi yetu atafanya hivyo.
Ndugu Wananchi;
Jambo la mwisho ambalo ningependa kuliongelea leo linahusu msiba uliotukuta wa Mbunge wa Tarime, Marehemu Chacha Wangwe.Kifo chake cha ghafla kimetushtua na kutusikitisha wengi. Marehemu alikuwa mtu muwazi na mkweli.Hakuwa na woga wa kutoa maoni yake kwa jambo analoliamini. Hakika Bunge,Jimbo la Tarime na Taifa limepoteza mwakilishi wa kutumainiwa. Daima atakumbukwa kwa sifa zake hizo na mchango wake huo kwa taifa.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuitumia nafasi hii kutoa mkono wa pole na rambirambi kwa familia na ndugu wa marehemu.Naelewa machungu mliyonayo.Mimi na Watanzania wote wenye nia njema tuko pamoja nanyi katika msiba huu mkubwa uliowakuta. Ni msiba wetu sote na ni machungu yetu sote.
Nawapa pole sana Wabunge wote wa Bunge letu tukufu kwa kupoteza mwenzi wenu na rafiki yenu. Nawapa pole viongozi na wanachama wa Chama cha CHADEMA kwa kupoteza kiongozi wenu mahiri.Wananchi wenzangu wa Jimbo la Tarime nao nawapa pole kwa kupoteza mwakilishi na mtetezi wenu shupavu.Tuzidi kumwombea kwa Mwenyezi Mungu ampe mapumziko mema.Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Kwa mara nyingine tena nawashukuru tena kwa msaada wenu na ushirikiano wenu. Mimi na wenzangu mliotupa dhamana ya kuliongoza taifa letu tutaendelea kuwatumikia kwa nguvu na uwezo wetu wote ili tufikie kwenye dhamira yetu ya kuharakisha maendeleo ya nchi yetu.
Kwa pamoja tutashinda.Mungu Ibariki TanzaniaMungu Ibariki Afrika.Asanteni kwa kunisikiliza.