WAZIRI
Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, ametoa dukuduku lake la moyoni akisema
hana uhasama na Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa na kubainisha
kuwa rushwa ya kimtandao iliyokighubika Chama cha Mapinduzi (CCM), ndiyo
iliyomwangusha wilayani Hanang’.
Sumaye ambaye amepigwa mweleka kwenye uchaguzi wa ujumbe wa Halmashauri
Kuu (NEC) Taifa kupitia wilayani Hanang’ na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Uwekezaji na Uwezeshaji), Mary Nagu, alikutana na wanahabari
kuelezea mwendo mzima wa uchaguzi huo na hatima ya CCM.
Akizungumza kwa kujiamini huku akinukuu kauli zake za nyuma kuhusu
mwenendo wa rushwa ndani ya chama chake, alisema uchaguzi wa Hanang’
ulighubikwa na matumizi makubwa ya rushwa, vitisho vingi, uharamia wa
kuhamisha wapiga kura usiku na maovu mengineyo mengi.
“La msingi ni kuwa mimi sijakata na wala sitakata rufaa ya kupinga
matokeo wala kupeleka malalamiko katika chama changu kwa sababu
yaliyokuwa yakitendeka yalikuwa yanafahamika,” alisema.
Katika kile kinachoweza kutafsiriwa kama kuondoa uvumi uliokuwepo kuwa
Sumaye na Lowassa wana ugomvi wa kisiasa hasa wakati huu wa kujipanga
kuelekea mbio za urais 2015, kiongozi huyo alisema hajazungumza na mtu
kuhusiana na mambo hayo.
Sumaye alisema taarifa hizo zimekuwa zikisambazwa na kunukuliwa kuwa
zimetoka kwenye chanzo kilicho karibu naye, lakini akafafanua kuwa
hawezi kupambana na Lowassa kwa sababu hana uhasama naye.
“Nikiamua kugombea urais sitagombea kwa sababu ya mtu fulani bali
nitagombea kwa sababu ya nchi na wananchi wa Tanzania,” alisema.
Akifafanua kuhusu vitendo vya rushwa ndani ya CCM, alisema kuwa nchi
nyingi hasa zenye demokrasia changa kama Tanzania zimeingia katika
vurugu na kuhatarisha amani na utulivu nyakati za uchaguzi.
Sumaye alisema madaraka yatakuja tu kama wananchi wapiga kura wanaona
wewe ndiye utayewafaa na wala wasirubuniwe kwa fedha au jambo lolote kwa
kutumia vibaya nafasi ya umaskini wao.
“Hivi leo tunavyoongea hali ya rushwa wakati wa uchaguzi imekuwa mbaya
zaidi. Katika uchaguzi wa kidemokrasia wapiga kura humchagua mwakilishi
wanayemtaka kwa sababu ya uwezo wake yaani humchagua mwakilishi wao kwa
ajili yao.
“Katika demokrasia iliyopondeka kwa rushwa, fedha huwachagulia watu
mwakilishi kwa ajili ya waliotoa fedha. Wapiga kura ni wapiga mihuri
tu,” alisema.
Sumaye bila kutaja majina ya wahusika, alisema hali imetoka kwenye
kuhonga ili achaguliwe katika eneo lake na badala yake kuna rushwa za
kimtandao ambapo mtu hutoa fedha katika maeneo mbalimbali nchini ili
watakaochaguliwa wawe wafuasi wake mbele ya safari atakapowahitaji.
“Uchaguzi huu umeghubikwa sana na matumizi makubwa ya fedha za rushwa.
Suala la rushwa katika nchi yetu na katika CCM siyo mgeni lakini sasa
tatizo hilo limeota mizizi na linazidi kuwa kubwa,” alisema. Kuhusu kwenda CHADEMA
Sumaye alikanusha vikali akisema hajawahi kukutana na kiongozi yeyote wa CHADEMA wala chama chochote cha upinzani.
Lakini akabainisha kuwa hawapaswi kufikia kudai kuwa vyama vya upinzani au viongozi wake ni maadui wa CCM.
“Mimi ningekuwa nimekutana nao ningesema tu mbona hata hao wengine
wanaoutafuta urais kwa udi na uvumba huwa wanakutana nao? Alihoji.
Alisema yeye ni mwanachama mwaminifu wa CCM na kwamba alishawahi kusema
kuwa hayuko kwa ajili ya cheo na wala kukosa ujumbe wa NEC na hasa kwa
njia iliyotumika hakumnyimi usingizi wala hahuzuniki kugombea urais kwa
tiketi ya CCM endapo ataamua kufanya hivyo.
Sumaye alisema kama ni matatizo, vyama vyote vina kasoro zake, hivyo
haoni kama kuhama chama ni suluhu na kutamba kuwa kushindwa kwake
kumempa nguvu zaidi na hivyo akiamua kugombea urais lazima apitie CCM. Kuhusu TAKUKURU
Alipoulizwa kuhusu utendaji wa Taaasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) kama imetimiza wajibu wake kushughulikia tuhuma za rushwa
kwenye uchaguzi wilayani Hanang’, Sumaye alitafakari kidogo kisha
akajibu kwa kutumia mfano.
“Hivi kama nyie wanahabari mmekuja hapa mkanisikiliza haya
ninayowaeleza, halafu kesho watu wanasoma kwenye magazeti yenu hawakuti
kitu au kwenye televisheni hawaoni, wanaweza kusema mmetimiza jukumu
lenu? Alihoji Sumaye.
Kada huyo aliwaachia wanahabari watafsiri wenyewe kama kweli TAKUKURU
inatimiza wajibu wake katika kushughulikia madai ya rushwa kwenye
chaguzi.
“Napenda nitambue kuwa haya ninayoyasema si matamu masikioni mwa baadhi
yetu lakini ni vema tukayasikiliza kwa makini na kuchukua hatua chanya
ili yasilete madhara zaidi katika jamii na wala tusidiriki
kuwanyamazisha wanaoyazungumzi |
|