Tuesday 8 September 2015

Wadau naomba mtumie Code kwa blog zetu, natanguliza shukran
Logo ya Zanzibar Diaspora Association (ZADIA)
Na Muandishi wetu swahilivilla Blog
Wanadiaspora wameelezea wasiwasi wao kuwa sheria mpya ya Makosa Ya Mtandao iliyoanza kufanya kazi tarehe mosi mwezi huu nchini Tanzania, huenda ikaishia Chumbe, imefahamika.
Hayo yamekuja kwenye kongamano maalum lililoandaliwa na Jumuiya Ya Wazanzibari Waishio nchini Marekani (ZADIA) kujadili Sheria Mpya ya Makosa Ya Mtandao na Athari zake Kisiasa.
Wageni rasmi katika kongamano hilo lililofanyika kwa njia ya simu walikua ni Mwandishi khabari Bi Salma Said, na Mwanadiplomasia mstaafu Bw. Muhammed Yussuf Mshamba.
Utata wa Kisheria:
Akizungumza kwenye kongamano hilo, Bi Salma Said alisema kuwa sheria hii itakuwa na utata kutokana na jinsi ya mchakato mzima wa kuipitisha ulivyokwenda. "Sheria imepitishwa kimabavu, kwani wadau wote hawakushirikiswa, pia ilipitishwa wakati Wabunge wa upinzani wakiwa wametoka Bungeni" alifafanua Bi Salma na kuongeza kuwa Baraza la Wahariri Tanzania liliikataa sheria hiyo na kupitisha azimio la kumshauri rais Kikwete asiitie saini, lakini Mheshimiwa rais aliitia saini.
Kwa upande wake, Bwana Muhammed Yussuf Mshamba ambaye pia ni Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alielezea wasiwasi wake juu ya uwezekano wa sheria hiyo kutekelezeka kwa vile mfumo uliotumika kuiptisha haukukidhi haja.
Akizungumza katika kongamano hilo, Bwana Mshamba ambaye aliwahi kuwa mtia nia wa kuwania urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM alisema "Sharia ile ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini Zanzibar hawakupata nafasi ya kuiangalia".
"Kwa mujibu wa kifungu cha 234 cha Katiba ya Zanzibar, sharia zote zinazopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ambazo zinatakiwa kutumika Zanzibar na Bara, kwa mujibu wa kipengele kile ni lazima Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lipewe nafasi ya kuziangalia". 
Alisema Bwana Mshamba na kuongeza kuwa, sheria ile ilipitishwa wakati Baraza la Wawakilishi limeshavunjwa na hakukuwa na njia ya kuliitisha angalau kwa kikao cha dharura ili kuweza kuijadili.
Kutokana na hali hiyo, Bwana Mshamba alisema kuwa, sheria ile kwa sasa haiwezi kutekelezeka Zanzibar mpaka Baraza jipya la Wawakilishi litakapochaguliwa na kuipitia. 
Alielezea sheria hiyo huenda ikapta upinzani katika Baraza jipya kwa vile mambo yaliyomo ndaniyake yana utata. "Tunajua kuwa swala la mawasiliano, ni swala la Muungano, lakini je ni kwa kiasi gani? Je swala la mtandao linaingia?" Alihoji mwanasiasa huyo, na kuongeza "Kwa mujibu nilivyoelewa, sharia ile ina mambo ya faragha, na Wazanzibari wanayo faragha yao, na wana mambo yao wanataka wayashughulikie wenyewe"
Alitoa wito kwa pande zote kukaa tena na kuipitia na kuijadili sheria hiyo ili kweza kukidhi haja ya kisheria na kuweza kutekelezeka bila kuleta madhara.
Kutokana na utata huo wa kisheria, Mwenyekiti wa Jumiya ya Watanzania katika jiji la Dallas Bwana Ben Kazora, alihoji uwezekano wa kuwakamata washukiwa wa makosa mtandao ikiwa sheria yenyewe haiwezi kutumika Zanzibar.
Ni sheria zipi zitakazotumika kuwakamata watuhumiwa, za Tanzania, za nchi watuhimiwa walizo au sheria za kimataifa za mtandao?' alihoji Bwana Kazora.
Uwezo Wa Kitaaluma
Licha ya serikali ya Tanzania kujipiga kifua kukhusu uwezo wake wa kusimamia sheria mpya ya Makosa ya Mtandao, washiriki katika kongamano hilo walielezea wasiwasi wao kuwa Tanzania ina uwezo mdogo kiteknolojia kuweza kuisimamia na kuitekeleza sheria hiyo kiutaalamu bila kuleta madhara kwa jamii.
Akichangia mada hiyo, mtaalamu wa sayansi ya kompyuta Dk Hassan Omar Ali, alisema kuwa Tanzania ina uwezo mdogo kiteknolojia kuweza kufuatilia kesi za aina hiyo, na hivyo kuna uwezekano wa watu kubambikizwa kesi na wakawa hawana uwezo wa kujitetea.
"Kama mnavyofahamu, mtu unawekwa ndani unaambiwa uchunguzi bado unaendelea, kwa mambo ambayo tayari tunayaweza, uchunguzi unaendelea kwa miaka, sikwambii kwa mambo ambayo hatuyawezi sasa hivi" alitoa changamoto Dk Hassan aliyeandika kitabu cha "Kompyuta: Jifunze na Ielewe"
Msomi huyo aliyewahi kuandika makala maarufu chini ya kichwa cha maneno: "mawasiliano ya mtandao hayana siri", alionya kuwa uwezekano wa mtu kuweza kukamatwa kwa makosa ya kimtandao upo, ispokuwa tu kwa Tanzania uwezo wake wa kiutaalamu na kifedha ni mdogo.
Mbali na khofu ya upungufu wa wataalamu wa maswala ya mtandao, wanadiaspora pia walielezea wasi wasi wao juu ya upungufu wa wataalamu wa sheria za mitandao nchini Tanzania.
Akitoa hoja katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania katika jiji la Dallas Bwana Ben Kazora, alielezea khofu yake kuwa upungufu wa wataalamu wa fani hiyo huenda ukaleta athari mbaya katika utekelezaji wa sheria hiyo.
"Je wataalamu wetu wako tayari kusimamia sheria hii?" Alihoji Bwana Kazora, na kuelezea khofu yake kuwa huenda swala hili likawa limechochewa kisisasa.
Kutumiwa vibaya sheria ya Mtandao.
Kwa upande mwengine, wazungumzaji katika kongamano hilo walielezea dukuduku lao kuwa sheria ya mtandao huenda ikatumika vibaya kwa malengo ya kisiasa au chuki binafsi.
Akifafanua baadhi ya vipengele vilivyomo katika sheria hiyo, Bi Salma Said ambaye pia ni mwanaharakati za kijamii, alisema kimantiki tunahitaji sheria kama hii kudhibiti matumizi mabaya ya mtandao, ispkuwa yaliyomo ndani yake yana utata.
"Katika ile sheria, kuna kipengele kinasema, polisi akikushuku tu anaweza kukwambia wende ukawasilishe simu yako Polisi, tena si kwa amri ya mahkama, ni yeye tu askari" alilalamika Bi Salma, na kuongeza kuwa, simu itaakapofika polisi haki ya faragha inapotea, kwani hujui ni nini kitakachopekuliwa katika simu yako.
Kutokana na hali hiyo, kuna uwezekano wa polisi kuitumia vibaya sheria hiyo ili kumtia mtu adabu kutokana na chuki binafsi, alionya Bi Salma.
Akijibu swali lililoulizwa kuhusu iwapo Bunge Maalum la Katiba lilitilia maanani maswala ya faragha, enzi za mtandao na kumlinda mwananchi dhidi ya ubabe wa Dola, Bi Salma ambaye alikuwa ni mnjumbe wa Bunge hilo alisema "swala la uhuru wa faragha tulilijadili katika Bunge la Katiba, ingawaje hatukwenda ndani kuhusu mambo ya mtandao", na kuongeza kuwa Katiba imeweka wazi haki zote za raia, na haki za uhuru wa faragha zimo kwenye rasimu zote za Tume ya Jaji Warioba.
Kwa upande wake, akijibu swali hilo, Bwana Muhammed Yussuf Mshamba ambaye alikuwa mjumbe wa Tume ya Jaji Warioba iliyokusanya maoni ya wananchi na kuandaa rasimu ya Katiba Mpya alisema "Katiba hata ya sasa inalinda haki zote za kiraia, lakini serikali imekuwa na desturi ya kupitisha sharia zinazokwenda kinyume na Katiba".
Alifafanua kuwa tatizo si Katiba, bali ni vyombo vinavyosimamia na kutelekeza Katiba, na kusisitiza imani yake kuwa sheria mpya ya Mtandao itapata upinzani mkubwa katika Baraza la Wawakilishi.
Naye Dk Hemed Suleiman, alitahadharisha kuwa sheria hii inairejesha nyuma Tanzania katika maswala ya kidemokrasia na haki za binadamu.
Akitoa maoni yake katika kongamano hilo, Dk Suleiman alisema "Nina wasiwasi kwamba tusipochukua tahadhari, hii sheria huenda ikatumika kidikteta, na itaturudisha nyuma kutoka hatua tuliyofikia kuelekea kwenye demkrasia zaidi, na matokeo yake ni kuibana demokrasia zaidi".
Alitahadharisha dhidi ya uwezekano wa wanasiasa kuitumia vibaya sheria hii kwa ajili ya kuwakandamiza mahasimu zao kisisasa.
Hoja hiyo pia iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia Na Maendeleo (CHADEMA) tawi la DMV nchini Marekani, Bwana Kalley Pandukizi ambaye alielezea wasiwasi wake kuwa sheria hii inaweza kutumika vibaya na kuwaathiri watu wengi ambao hawana uelewa wa kutosha wa sheria hiyo.
"Wasiwasi wangu ni kuwa hizi sheria zitakapoanza kutumika zitakuja kuwaathiri watu ambao hawahui athari za hiyo sheria" alisema Bwana Pandukizi na kuendelea kuwa "Ndiyo maana baadhi ya wanasiasa wameingia wasiwasi na khofu kuwa sheria hii huenda ikiawa imetengenezwa makhasusi kwa ajili ya kuweza kuwatisha watu khususan katika harakati hizi za kisiasa zinazoendelea". Aidha mwanasiasa huyo wa CHADEMA alionya kuwa sheria mpya inakwenda kinyume na haki ya uhuru wa vyombo vya khabari na watu kujieleza.
Elimu Kwa Jamii.
Licha ya kuikosoa sheria mpya ya Makosa Ya Mtandao, hata hivyo wazungumzaji katika kongamano hilo liloandaliwa na ZADIA, walikubaliana kuwa iko haja ya kuwa na sheria kama hiyo, lakini isiwe imetokana na utashi wa kisiasa. Aidha walisisitiza umuhimu wa sheria kama hiyo kupitia taratibu zote za kimsingi kabla ya kupelekwa Bungeni. Moja kati ya kasoro za sheria hizo ni ukosefu wa elimu kwa wadau wote.
"Kwa kawaida, sharia kabla haijapitishwa hufanyika semina, lakini sidhani kuwa hilo lilifanyika" Alisema Kada wa CCM, Bwana Muhammed Yussuf Msahamba, na kuongeza kuwa ikiwa kweli viongozi wetu walikuwa na nia ya kulinda mila, silka na tamaduni zetu, basi hakukuwa na haja ya sheria kama hiyo kupitishwa kwa hati ya dharuara.
Akijibu swali kuhusu nini Wanadiaspora wanaweza kufanya kuhusiana na sheria hii mpya, Bwana Mshamba alisema kuwa Wanadiaspora wanaweza kutoa mchango mkubwa kwa kusaidia kutoa elimu kwa jamii kwa kupitia njia mbalimbali.
"Mumanyo nafasi nzuri ya kuchangia, kwa njia za makongamano kama hili kuzipitia sharia na kuzichambua" alisema bwana Mshamba na kuongeza kuwa Wanadispora wanaweza pia kulinganisha sheria za nchi wanazoishi na kupeleka uzoefu wao nyumbani kwa kushirikiana na Taasisi za kizalendo.
Kwa upande wake, akijibu swali hilo, Bi Salma Said alisema "Elimu ni muhimu. Ni vizuri kuipitia sheria na kutoa taaluma kwa jamii". Na kusisitiza kuwa mwamko na uelewa kwa jamii yetu ni mdogo khususan katika mswala ya mitandao ya kijamii na sheria zake.