Wednesday 2 September 2015


Mwaka 2004, John Kitime ambaye kwa sasa ndie Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanamuziki Tanzania (Tanzania Musicians Network-TAMUNET) alihudhuria Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Muziki Duniani –International Federation of Musician (FIM). Katika mkutano huo moja ya maazimio ya mkutano ule ilikuwa kila nchi ihakikishe inaanzisha utaratibu wa Bima ya Afya kwa wanamuziki wake. 

Mara baada ya kurudi Tanzania, kwa kushirikiana na viongozi wengine wa TAMUNET, Kitime alianza kufuatilia uwezekano wa kupata huduma ya Bima hiyo kwa wanamuziki. Kwa bahati mbaya hakukuwa na njia yenye gharama nafuu ya malipo ya BIma hiyo ambayo mwanamuziki wa kawaida angeweza kuyamudu. Kulikuweko na kampuni ambayo iliweza kutoa huduma hiyo kwa gharama ya dola 300 kwa mwaka kwa mwanamuziki mmoja. Kampuni nyingine za Bima zilizotembelewa hazikuonyesha ushirikiano katika jambo hilo. TAMUNET iliwasiliana pia na mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa katika kipindi hico mfuko ulikuwa hauna mamlaka ya kuhudumia watu waliokuwa nje ya ajira ya serikali na mashirika ya umma. TAMUNET iliwasiliana na Mganga Mkuu wa Serikali, ambaye alishauri TAMUNET kuwasiliana na NGO moja ambayo ilikuwa na makao yake makuu Sinza, na kweli NGO hiyo ilikubali kuwa ingeweza kutoa huduma ya Bima ya Afya kwa wanamuziki kwa gharama ya shilingi 3000/- tu kwa mwezi, lakini huduma hii ilikuwa ni kwa hospitali kadhaa tu jijini Dar es Salaam. Hilo nalo lilionekana ni bora kuliko kukosa kabisa, lakini muda mfupi baadae NGO hiyo ilisema haishughuliki tena na huduma hiyo bali imeelekeza nguvu zake kwa watoto wa mtaani. Hapo ilifuatia miaka kadhaa ambayo hakukuweko na njia yoyote iliyowezekana ya kupata huduma hiyo. TAMUNET ilijaribu pia kuwasiliana na mifuko mingine, lakini kila mara iligonga ukuta aidha kwa ahadi ambazo zilikuwa zikipigwa kalenda bila kutekelezwa.

Mwaka 2015 hatimae ndipo mlango umefunguka, Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa NHIF, uliitarifu TAMUNET kuwa umeanzishwa mpango wa Bima kwa Kikoa ambao ungewawezesha wanamuziki nao kupata Bima ya Afya kwa gharama nafuu. TAMUNET iliuchangamkia mpango huo kwa kuwa imekuwa ajenda ya chama hiki kwa miaka zaidi ya kumi.

Wanamuziki wanachama wa TAMUNET tayari wameanza kufaidi huduma ya Bima ya Afya kwa mwaka mzima, hii ni baada ya kulipia shilingi 76,800/-. Mpango huu utaondoa aibu ya wanamuziki kuchangiwa fedha za matibabu kila wanapougua, kwani itakuwa busara kwa wapenzi na washabiki wa muziki kuchangia mwanamuziki wanaempenda apatiwe Bima ya Afya kuliko kumchangia fedha za matibabu ya muda mfupi. Baadhi ya wanamuziki ambao tayari wana bima za afya chini ya mpango huu ni Louiza Nyoni, Abdul Salvador, Rashid pembe, na wengine wengi wamekwisha anza taratibu za kupata huduma hii.
Wasanii katika semina kuhusu BIma Ya Afya iliyofanyika BASATA karibuni

Muwezeshaji Catherine kutoka Mfuko wa Taifa wa BIma ya Afya akitoa maada katika semina ya wasanii kuhusu Bima ya Afya

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Paul Makond aliyekuwa mgeni rasmi katika semina ya Bima ya Afya kwa wasanii

Mwenyekiti wa TAMUNET akipokea kadi za kwanza za Bima ya Afya za wanamuziki, katika ofisi za Mfuko wa BIma ya Afya wa Taifa.

John Kitime akiwa na kadi yake ya BIma ya Afya aliyoipata karibuni

Kadi za Bima ya Afya za wanamuziki mbalimbali



Louiza Nyoni akionyesha kadi yake mpya ya Bima ya Afya
Ushirikiano wa Mfuko wa Biam ya Afya na TAMUNET unaweka uwezekano wa mwanamuziki kuanza kuchanga hata fedha kidogokidogo ili kuweza kufikisha kiasi kinachotakiwa. Wanamuziki wanaweza kupiga simu au kutuma ujumbe kwenue simu na 0763722557 ili kupata maelezo ya namna ya kujiunga na huduma hii. Ukiwa mwanamuziki wa Hiphop, taarab, muziki asili, dansi bongofleva, huduma hii ni kwa ajili yako kumbuka WAJANJA HUJIWEKEA BIMA YA AFYA- NA WEWE NI MMOJA WA WAJANJA