Wednesday 9 October 2013

Katika Gazeti la Mawio Toleo Namba 0062 la tarehe 26.9.2013 – 02.10.2013 na toleo Namba 0063 la tarehe 03.10.2013 zimechapishwa habari zenye vichwa vya habari "Mtandao wa Ujangili Huu Hapa" na "Wabunge CCM watajwa ujangili".

Katika habari zote hizo zimelihusisa shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kama chanzo cha habari hizo.

Shirika la Hifadhi za Taifa linapenda kutoa ufafanuzi ufuatao kuhusiana na taarifa hizi:
(i) Shirika la Hifadhi za Taifa halijawahi kudhamini ripoti iliyotajwa katika habari hizo kuhusiana na utafiti makini wa ujangili.

(ii) Shirika husimamia shughuli za uhifadhi katika maeneo ya Hifadhi za Taifa pekee kiutendaji, ambapo baadhi ya maeneo yaliyotajwa katika habari hizo kama Selous na Liwale kiutendaji hayapo ndani ya Shirika la Hifadhi za Taifa.

(iii) Kama Shirika la Umma, hufuata taratibu za kisheria ikiwa ni pamoja na kushirikisha vyombo mbalimbali vya dola katika kushughulikia uhalifu wa aina mbalimbali ikiwemo ujangili.

Ni kwa mantiki hii basi, shirika linapenda kuweka bayana kuwa halihusiki na taarifa hizo, na hata pale zinapopokelewa zina utaratibu wake wa kufanyia kazi.

Tunachukua nafasi hii kuviomba vyombo vya habari kushiriki katika juhudi za kupambana na ujangili kwa kuwa waangalifu katika kuandika habari za kutuhumiana kabla ya kuwa na ushahidi kamili ambao ni haki ya kimsingi ya kisheria inayopaswa kuheshimiwa.

Imetolewa na Idara ya Uhusiano
HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA