Tuesday, 13 October 2015

BENKI KUU YA TANZANIA YAANZISHA MFUMO MPYA WA MALIPO KWA MASAA 24 UTAJULIKANA KAMA TISS.


 Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bernard Dadi (kulia), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo mchana, kuhusu benki hiyo kuanza kutumia mfumo wa malipo baina ya benki na benki kwa masaa 24 kwa siku saba za wiki kwa mwaka utakajulikana kama TISS. Kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki, Marcian Kobello.
 Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki, Marcian Kobello (kushoto), akizungumza katika mkutano huo.
 Waandishi wa habari wakichukua taarifa hiyo.
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea. Walioipa kamera mgongo kutoka kushoto ni Meneja Msaidizi wa Idara ya  Uhusiano wa benki hiyo, Vicky Msima na kulia ni Kaimu Meneja Huduma za Kibenki, John Kayombo.

Na Dotto Mwaibale

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imesema kuanzia mwakawa fedha ujao itaanza kutumia mfumo wa malipo baina ya benki na benki kwa masaa 24 kwa siku saba za wiki kwa mwaka ambapo utakuwa ukijulikana kama TISS.

Hayo yamesemwa Dar es Salaam leo  mchana na Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo BoT, Bernard Dadi na kuongeza mfumo huo utaweza kufanya kazi kwa ufanisi iwapo wafanyabiasha na wananchi kwa ujumla watauchangamkia kwani kwa sasa inapatikana kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa mbili usiku kwa benki za kibiashara zilizojiunga.

"Kwa sasa kuna mfumo huu wa TISS ambao umekuwa ukifanya kazi siku za kazi hadi saa mbili usiku na siku za mapumziko na sikukuu unafanya kazi kuanzia saa tatu hadi saa nane, ila tunatarajia mwaka wa fedha ujao utakuwa unafanya kazi kwa masaa 24," alisema.

Alisema kimsingi mfumo huo una lengo la kuondoa mfumo wa kutumia hundi ambao unatumia muda mrefu na wakati mwingine kuna makosa ambayo yanatokea ya mtu anavyoandaa hivyo kuchelewa.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki wa BoT, Marcian Kobello alisema uhaba wa sarafu ya shilingi 500 mitaani unachangiwa na wananchi wenyewe ambao wakienda benki hawachukui fedha hizo hivyo kusababisha zibakie huko kwenye mabenki.

Alisema sarafu za shilingi 500 zipo zaidi ya milioni 100 BoT lakini hadi sasa ni milioni 20 ndizo zipo katika mzunguko hali ambayo inachangia kuadimika kwa fedha hizo.

Alitoa mwito kwa wananchi na wafanyabiashara kuchukua sarafu hizo katika mabenki ili ziweze kufika katika mizunguko na dhana kuwa sarafu hiyo ina madini ya fedha ni uongo kwani asilimia 94 ni chuma na asilimia 6 ni nikoni.

Aliwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kupeleka fedha ambazo zimechakaa katika mabenki ili waweze kubadilishiwa kwani utaratibu wa kuuza fedha haupo kisheria pamoja na ukweli kuwa hakuna sheria inayokataza.