Wednesday 3 September 2014

 Rais Jakaya Kikwete akizungumza na wananchi hivi karibuni   
---
   Na Habel Chidawali, Mwananchi
Rais Jakaya Kikwete amesema zaidi ya asilimia 80 ya ahadi alizotoa wakati anaingia madarakani zimetimizwa na zilizobakia atazimaliza kabla ya kuondoka madarakani. 

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo juzi katika Kijiji cha Gulwe, Mpwapwa mkoani Dodoma, alipokwenda kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja.
Alisema wakati anaingia madarakani mwaka 2005, alitoa ahadi mbalimbali katika maeneo tofauti zikiwamo zilizoandikwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambazo zimeendelea kutimizwa kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha.
“Sasa tumefikia asilimia 80 ya utekelezaji wa ahadi zetu, naamini tunaweza kufanikiwa kwa zote na kama tutashindwa basi tutaacha kidogo sana, lakini kumbukeni tumetekeleza hata yale ambayo hayakuwa katika ahadi,” alisema Rais Kikwete.
Akizungumzia daraja hilo la Gulwe, aliwaagiza makandarasi kufanya kazi usiku na mchana ili likamilike kama ilivyopangwa.Alisema wananchi wanataka kuona kazi hiyo inakwisha.