Friday 4 January 2013


 
 Mtu aliyejitambulisha kuwa askari wa Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ),kambi ya Monduli,Arusha kwenye mkutano wa Chadema Mji mdogo Mererani,Simanjiro mkoani Manyara hivi karibuni akiwa ndani ya gari ya jeshi baada ya kutiwa nguvuni, 
 
  Picha juu alipopiga picha na Viongozi mbalimbali wa Chadema
Mtu aliyejitambulisha kuwa askari wa Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ),kambi ya Monduli,Arusha akiwa na wabunge wa Chadema, Godbless Lema (Arusha Mjini) na Joshua Nassari (Arumeru Mashariki) baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara uliohutubiwa na wabunge hao katika Mji mdogo Mererani,Simanjiro mkoani Manyara hivi karibuni.
---
Yule mtu aliyedaiwa kuwa ni mwanajeshi wa JWTZ wa kikosi cha Monduli ametiwa mbaroni leo kwa ushirikiano wa jeshi la wananchi na Police.

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa kijana huyu hakuwa mwanajeshi wa JWTZ kama alivyojitambulisha kwa waandishi wa habari, ila aliwahi kuwa JKT na akaacha. Amekuwa akivaa ngua hizo za jeshi kwa miaka mingi na wananchi wa Mererani wanamtambua kama mwanajeshi.Kujua Habari zaidi jinsi mambo yalivyokua Bofya Hapa na Hapa.......>>>




Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo (Mb)
--
1.0 UTANGULIZI
Wizara ya Nishati na Madini inapenda kutoa ufafanuzi wa miradi ya Gesi  Asilia ambayo itatekelezwa kwa kushirikiana na wawekezaji katika Sekta ndogo ya Gesi Asilia na kueleza manufaa makubwa yatakayopatikana kwa wananchi wote wa Tanzania wakiwemo wale wa Mikoa ya Mtwara na Lindi. 

Siku ya Alhamisi, tarehe 27 Disemba 2012, baadhi ya Vyama vya Siasa vya Upinzani viliratibu na kuhamasisha baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara, wengi wao wakitokea Mtwara Mjini kufanya maandamano ya kudai raslimali ya Gesi Asilia iwanufaishe wakazi wa Mtwara na kupinga mradi mkubwa wa ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Wizara ya Nishati na Madini inapenda kutoa taarifa ifuatayo kwa Wa-Tanzania wote kwa kupitia vyombo vya habari.

Tokea Uhuru, uchumi wa Tanzania umetegemea kilimo cha mazao ya biashara kama vile katani (Tanga na Morogoro), pamba (Mwanza, Mara na Shinyanga), kahawa (Kilimanjaro, Kagera, Ruvuma na Mara),  chai (Iringa) na tumbaku (Tabora). Fedha za mazao haya zimewanufaisha wakazi wa mikoa yote ya nchi yetu  bila ubaguzi wo wote wala wakulima wa kutoka mikoa hiyo hawajawahi kufanya maandamano wakidai upendeleo (dhidi ya Wa-Tanzania wengine) wa aina yo yote ile.  

1 Mapato  yatokanayo na uchimbaji wa dhahabu (Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga na Tabora), almasi (Shinyanga) na tanzanite (Manyara) yamewanufaisha Wa-Tanzania wote bila ubaguzi wo wote ule! Minofu ya samaki wa Ziwa Victoria (Mara, Mwanza na Kagera) imeliingizia Taifa letu fedha nyingi ambazo zimetumiwa na wakazi wa nchi nzima bila ubaguzi wowote. 

Aidha kuna mikoa ambayo inazalisha mazao ya chakula kwa wingi kwa manufaa ya Wa-Tanzania wote.Mahindi kutoka Rukwa,Mbeya, Ruvuma na Iringa yanasafirishwa kwenda mikoa yote ya nchi yetu bila kujali eneo yanakolimwa na wakazi wa mikoa hiyo hawajawahi kudai mahindi hayo ni kwa ajili ya watu wa mikoa hiyo pekee. Sukari ya Kilombero, Mtibwa na Kagera inatumiwa na wakazi wa mikoa yetu yote bila ya kuwepo madai ya mikoa inayozalisha sukari hii kupewa upendeleo wa aina yo yote ile. Maji ya Mto Ruvu yanatumiwa na wakazi wa Dar Es Salaam bila manung’uniko yo yote kutoka kwa wakazi wa eneo la chanzo cha Mto Ruvu. 

Umeme wa kutoka Mtera, Kidatu na Kihansi (Dodoma na Morogoro), Hale (Tanga), na Nyumba ya Mungu (Kilimanjaro) unatumiwa na wakazi wote wa Tanzania bila ubaguzi au malalamiko ya wenyeji wa sehemu ambazo umeme huo unafuliwa na kusafirishwa kwenye Gridi ya Taifa. 

Kwa hiyo, kutokana na mifano hii michache, ni wajibu wa wazalendo na wapenda maendeleo wa kweli na hasa Wa-Tanzania wanaopinga ubaguzi wa aina yo yote ile kujiuliza kwa kina sababu zilizopelekea Vyama Siasa vya Upinzani kupanga, kuhamasisha, kushabikia na kuongoza maandamano ya tarehe 27 Disemba 2012 pale Mtwara Mjini.  

2.0 RASLIMALI YA GESI ASILIA TANZANIA
Gesi Asilia ilianza kugundulika hapa nchini tangu mwaka 1974 kwenye Kisiwa cha Songo Songo, Mkoani Lindi. Baada ya hapo Gesi Asilia imegundulika maeneo ya Mtwara Vijijini, yaani Mnazi Bay (1982) na Ntorya (2012), Mkuranga (Pwani, 2007), Kiliwani (Lindi, 2008). Kiasi cha Gesi Asilia iliyogunduliwa katika maeneo haya inakadiriwa kuwa Futi za 

2 Ujazo Trilioni 4.5 – 8. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kumekuwa na kasi kubwa ya utafutaji Mafuta na Gesi Asilia uliojikita zaidi kwenye maji ya kina kirefu cha bahari. Kiasi cha Gesi Asilia iliyogundulika katika kina kirefu cha maji inafikia takribani Futi za Ujazo Trilioni 27. Kiasi cha wingi wa Gesi Asilia yote iliyogunduliwa nchi kavu na baharini inafikia takribani Futi za Ujazo Trilioni 35.  

Kufuatana na Sheria za nchi yetu zinazotumiwa kugawa mipaka ya mikoa iliyopo kando kando mwa bahari (isivuke 12 nautical miles au 22.22 km kuingia baharini), Gesi Asilia iliyogunduliwa hadi sasa katika Mkoa wa Mtwara pekee ni asilimia 14 tu ya gesi yote iliyogundulika nchini. Kwa kutumia kigezo hicho cha Sheria za mipaka ya ki-utawala ya mikoa yetu, Lindi inayo 7% ya gesi yote, Pwani 1% na huku Kina Kirefu cha Bahari (Deep Sea) ndicho chenye gesi nyingi (78%) kuliko mikoa yote ikiwekwa pamoja! Kwa hiyo, hakukuwa na haja ya kufanya maandamano kwa sababu Gesi Asilia nyingi inapatikana kwenye bahari ya kina kirefu ambayo iko ndani ya mipaka ya nchi yetu bila kujali mipaka ya mikoa yetu. Isitoshe Gesi Asilia imegundiliwa kwenye miamba tabaka (sedimentary rocks) yenye umri wa Miaka kati ya Milioni 199.6 hadi 23.03. Mipaka ya Bara la Afrika, ya nchi yetu na ile ya mikoa yetu haikuwepo wakati huo!  

Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia pia unaendelea tukiwa wa mategemeo makubwa ya upatikanaji wa raslimali hizi katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Manyara, Kigoma, Mbeya, Njombe, Rukwa, Katavi, Morogoro na Tabora pamoja na kwenye kina kirefu cha maji baharini kuanzia mpaka wetu na Msumbiji hadi mpaka  wetu na Kenya. Hatutarajii mikoa hii nayo ifanye maandamano ya kutaka kuhodhi raslimali za Gesi Asilia na Mafuta zitakapogunduliwa mikoani mwao. 

3.0 MATUMIZI YA GESI ASILIA YA MNAZI BAY (MTWARA) NA SONGO SONGO (LINDI) 
Mpaka hivi sasa Gesi Asilia inayozalishwa na kutumika nchini ni kutoka Mnazi Bay (Mtwara Vijijini) na Songo Songo (Kilwa, Lindi). Gesi ya Mnazi Bay kwa sasa huzalisha umeme kwa ajili ya Mikoa ya Mtwara na Lindi tu. Mitambo ya kufua umeme kutokana na Gesi Asilia iliyopo Mtwara Mjini inao uwezo wa kuzalisha MW 18 lakini matumizi ya umeme ya Mikoa ya Mtwara na Lindi haijavuka MW 12. Umeme huo wa Mtwara unafuliwa na TANESCO huku Kampuni za Wentworth na Maurel & Prom zikizalisha Gesi Asilia  (inayotumiwa na TANESCO) kiasi cha Futi za Ujazo Milioni 2 kwa siku. Ikumbukwe kwamba ufuaji wa umeme wa hapo Mtwara Mjini ulikuwa mikononi mwa Kampuni ya Artumas iliyofilisika. 
Tangu Desemba 2006 hadi leo hii kiasi cha gesi kilichotumika kufua umeme kwa ajili ya mikoa hiyo miwili ni chini ya asilimia 1 ya gesi yote iliyogundulika Mnazi Bay (Mtwara Vijijini). Vilevile ikumbukwe kwamba kuna visima vinne vya Gesi Asilia pale Mnazi Bay (Mtwara Vijijini) na kinachotumika kwa sasa na tena kwa kiwango cha chini kabisa ni kimoja tu!  

Aidha ni vizuri ndugu zangu Wa-Tanzania wakaelewa kuwa Gesi Asilia hii inatafutwa na kuchimbwa na wawekezaji wenye mitaji mikubwa, wataalamu na teknolojia ya utafutaji na uchimbaji wa Gesi Asilia ambao wanapaswa kurejesha mitaji yao. Uchorangaji wa kisima kimoja cha utafutaji wa Gesi Asilia nchi kavu unahitaji Dola za Marekani Milioni 40, na kwenye kina kirefu cha maji baharini zinahitajika zaidi ya Dola za Marekani Milioni 100. Ikumbukwe kwamba, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Mafuta la Tanzania (TPDC), inatumia fedha za walipa kodi wa nchi nzima kwa shughuli za kuvutia, kuratibu na kusimamia utafutaji na uendelezaji wa Gesi Asilia nchini kote ikiwemo Mikoa ya Mtwara na Lindi. Walipa kodi Wa-Tanzania bado hawajalalamika wala hawajafanya maandamano ya kudai  fedha zao za kodi zisitumike huko Mtwara! 

Ni muhimu pia tukaelewa kwamba Gesi Asilia iliyopo Mnazi Bay (Mtwara Vijijini) inazalisha umeme peke yake kwa ajili ya Mikoa ya Mtwara na Lindi. Gesi Asilia ya Songo Songo (Kilwa, Lindi) ndiyo inayotumika kuzalisha umeme kwa ajili ya Gridi ya Taifa, na pia kwa ajili ya wananchi wa Kisiwa cha Songo Songo (Lindi), maeneo ya Somanga 

4 Fungu (Lindi) na viwandani (Dar Es Salaam). Tangu Oktoba 2004 ambapo mitambo ya kufua umeme ilipoanza kazi hadi leo hii, kiasi cha Gesi Asilia ya Songo Songo kilichotumika ni asilimia 7 tu ya Gesi Asilia yote iliyogunduliwa huko. Kwa hiyo, takwimu zinaonyesha kwamba hata uchumi wa Jiji la Dar Es Salaam unatumia kiasi kidogo sana cha Gesi Asilia (7%) iliyopo Songo Songo (Kilwa, Lindi). Ikumbukwe kwamba waajiriwa kwenye viwanda vya Dar Es Salaam wamo wanyeji wa kutoka Mtwara Mjini ambako maandamano yalifanyika na vilevile wamo wafanyakazi ambao ni wanachama wa Vyama vya Siasa vya Upinzani vilivyopanga, ratibu na kushabikia maandamano ya Mtwara Mjini ya tarehe 27 Disemba 2012. 

4.0 MIPANGO YA MATUMIZI YA GESI ASILIA KATIKA KIPINDI CHA MIAKA 5 HADI 10
(a) Ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia hadi Dar Es Salaam: 
Kuuza Gesi Asilia Jijini Dar es Salaam, kitovu cha uchumi wa Tanzania (80% ya mapato ya nchi yetu yanazalishwa Dar Es Salaam) ni uamuzi mzuri wa ki-uchumi. Tayari kuna viwanda 34 vinatumia Gesi Asilia  ambavyo vinahitaji kupanua shughuli zao endapo gesi zaidi itapatikana. Soko kubwa la Gesi Asilia lipo tayari Dar es Salaam (na siyo Mtwara), ambapo ipo mitambo ya kufua umeme kwa kutumia mafuta. Serikali inatumia fedha nyingi za kigeni kununulia mafuta ya kufua umeme tunaoutumia kila siku. 
Takribani  Dola za Marekani Bilioni Moja (sawa na Shilingi Trilioni 1.6) kwa mwaka zitaokolewa kutokana na mitambo iliyopo nchini ikifua umeme kwa kutumia Gesi Asilia na kuachana na mafuta ambayo ni ya bei kubwa sana. Bei ya umeme kwa uniti moja (KWh) ya umeme unaofuliwa kutumia dizeli na mafuta ya aina nyingine ni kati ya Senti za Marekani 30 hadi 45 na huku bei ya  uniti moja hiyo hiyo ni Senti za Marekani 6-8 kwa umeme utokanao na Gesi Asilia na zinapungua na wakati wa matumizi. Vilevile, takribani Dola za Marekani millioni 202 kwa mwaka zitaokolewa iwapo Jiji la Dar Es Salaam litatumia Gesi Asiliabadala ya mafuta katika magari, taasisi na majumbani. 

5.Fedha  hizi zikiokolewa zitatoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa Taifa letu kwa manufaa ya Wa-Tanzania wote wakiwemo wale waliondamana na wale walioratibu maandamo ya Mtwara Mjini ya tarehe 27 Disemba 2012. 

(b) Umeme mwingi zaidi kutokana na Gesi Asilia:
 Bomba la Gesi Asilia linalojengwa litasafirisha gesi nyingi zaidi ambayo itawezesha mitambo mipya itakayojengwa Kinyerezi (Dar Es Salaam) kufua umeme wa zaidi ya MW 990. Umeme mwingine utafulia Somanga Fungu (Lindi) wa kiasi kisichopungua MW520.

(c)  Usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini mwetu:
Dar es Salaam ndiko  kuna miundombinu mikubwa ya usafirishaji na usambazaji wa umeme kuliko mikoa mingine yote, hivyo ni uamuzi wa ki-uchumi unaotulazimisha kusafirisha Gesi Asilia kutoka Mikoa ya Lindi na Mtwara na kuipeleka Dar Es Salaam ambako itatumika kufua umeme, na kutumika moja kwa moja viwandani, majumbani na kwenye magari. 

(d)  Kwa kuzingatia mahitaji ya Gesi Asilia yatakayojitokeza:
Bomba  la kusafirisha gesi litawekewa matoleo ya kuchukulia gesi (tie-off) katika maeneo ya Mtwara, Lindi, Kilwa na Mkuranga ili kuhakikisha kuwa miji hii inakuwa na Gesi Asilia ya uhakika wakati wowote itakapohitajika. Kwa hiyo kuweka mitandao ya usambazaji wa gesi kutoka kwenye Bomba la Gesi Asilia linalojengwa kutarahisisha matumizi ya Gesi Asilia viwandani na majumbani katika Mikoa ya Mtwara na Lindi, na kwenye mikoa mingine kwa siku za baadae. 

(e) Serikali  imetenga  maeneo katika pwani ya Mikoa ya Kusini (Lindi na Mtwara) kwa ajili ya uanzishwaji wa maeneo ya viwanda (Industrial Parks/Estates)  vikiwemo viwanda vya
mbolea, Liquefied Natural Gas (LNG) na Petrochemicals. Ujenzi wa kiwanja cha sementi uko katika hatua za mwisho za maandalizi. 

(f) Ili kutengeneza mazingira mazuri ya biashara ya Gesi Asilia na Mafuta kwa kampuni za huduma, malighafi na vitendea kazi, Serikali imetenga eneo maalumu Mtwara, ambalo litawekewa miundombinu ya msingi ili kutoa vivutio mbalimbali kwa makampuni hayo. Eneo hilo litapewa hadhi ya Ukanda Huru wa Bandari (Freeport Zone). 

Ni lazima shughuli za kusafisha na kusafirisha Gesi Asilia zitatoa ajira katika maeneo husika. Kwa mfano kwa mitambo ya kusafishia gesi inayojengwa Madimba (Mtwara Vijijini) na SongoSongo (Kilwa, Lindi), kila mtambo utahitaji wafanyakazi na wengine watatoka Mikoa ya Lindi na Mtwara.  

Watanzania wanakumbushwa kuwa raslimali zilizopo nchini ikiwemo gesi asilia, madini, makaa ya mawe, wanyama pori, misitu, milima ya utalii, mito, maziwa, bahari n.k ni za Wa-Tanzania wote kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Raslimali hizi zinapatikana, zinatunzwa na kuzalishwa maeneo mbalimbali nchini mwetu na mapato yake yanatumika kwa maendeleo ya Wa-Tanzania wote bila kujali maeneo raslimali hizo zilipo. 

Tusikubali kuvunja nchi yetu vipande vipade kwa kisingizio cha raslimali zilizopo mikoani mwetu. Tusikubali kuvunjavunja mikoa yetu kwa kisingizio cha raslimali zilipo kwenye wilaya zetu.Tusikubali kuvunjavunja wilaya zetu kwa kisingizio cha raslimali zilizopo kwenye tarafa zetu. Tusikubali kuvunjavunja tarafa zetu kwa kisingizio cha raslimali zilizopo kwenye kata zetu. Tusikubali kuvunjavunja kata zetu kwa kisingizio cha raslimali zilizopo kwenye vijiji vyetu na mitaa yetu.

MUNGU IBARIKI TANZANIA, DUMISHA UHURU NA UMOJA WETU

Prof Dr Sospeter Muhongo (Mb)
WAZIRI YA NISHATI NA MADINI 
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA




Source: HAKI  NGOWI