Sunday 8 March 2015

YANGA NA SIMBA HAPATOSHI UWANJA WA TAIFA JIJINI DAR ES SALAAM JIONI YA LEO, JE, NANI KUIBUKA KIDEDEA?

Mar 8, 2015
Wakati joto la mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga, itakayopigwa leo Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, likiwa juu kadiri inavyokaribia kipute hicho kuanza saa kumi jioni hii, swali lililopo katika kila shabiki wa soka nchini na duniani kote ni je timu gani itafanikiwa kuwapaisha mashabiki wake kwa kutoka na ushindi Uwanjani?  
Mchezo huo utakaochezeshwa na Mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro, akisaidiwa na Soud Lila kutoka Dar es Salaam, mshika  kibendera wa kwanza, Florentina Zabron (Dodoma) mshika kibendera wa pili, Mwamuzi wa akiba ni Israel Mjuni, na kamisaa wa mchezo ni Ame Santimeya wote kutoka Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), viingilio vya mchezo huo,  VIP A sh. 40,000, VIP B sh. 30,000, VIP C sh. 20,000, Rangi ya Machungwa (Orange) sh. 10,000, huku Rangi ya Bluu na Kijani ikiwa ni sh. 7,000.
Tiketi zilianza kuuzwa jana (jumamosi) saa 2 kamili asubuhi katika vituo vya,  Karume (Ofisi za TFF), Mgahawa wa Steers (Posta Mpya), Oilcom (Buguruni), BigBon (Kariakoo),  Olicom (Ubungo), Dar Live (Mbagala), Uwanja wa Uhuru, Kivukoni (Ferry) na Makumbusho (kituo cha mabasi).
Magari yenye vibali maalum ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia ndani ya uwanja siku ya jumapili kwa kupitia barabara ya Mandela na Uwanja wa Uhuru, barabara ya Chang’ombe itafungwa kuanzia saa 12 kamili asubuhi.
TFF inawaomba, wapenzi, washabiki na wadau wa mchezo kununua tiketi katika vituo vilivyotajwa ili kuepuka kuuziwa tiketi bandia, ili kuimarisha ulinzi na usalama wa mchezo, mashabiki wenye mabegi, silaha, vilevi na chupa za maji hawataruhusiwa kuingia navyo uwanjani.
Aidha, katika mchezo huo TFF itatoa ujumbe maalum kupitia kwa wachezaji kuhamasisha juhudi za Taifa za kuzuia mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino).

RAIS KIKWETE AHUDHURIA MKUTANO KUJADILI MIRADI ILIYOKO UKANDA WA KASKAZINI, JIJINI KIGALI, RWANDA, AREJEA NYUMBANI

 Mwenyekiti wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea kwa furaha  sahada la maua baada ya kuwasili Kigali, Rwanda, tayari kwa mkutano  na viongozi wenzake wa Jumiya hiyo katika mkutano wa tisa wa wakuu wa nchi hizo kujadili miradi iliyoko katika Ukanda wa Kaskazini (Northern Corridor Integration Projects)  katika Hoteli ya Serena mjini Kigali. 
Mkutano wa leo ​pia umehudhuriwa na wakuu wa nchi za Kenya, Uganda na wenyeji Rwanda. Mbali na nchi hizo na mbali na Tanzania, nchi za Burundi na Sudan Kusini pia zili​alikwa kuhudhuria mkutano huo. Mkutano huo ni ulijadili hatua za utekelezaji wa miradi mbali mbali iliyokubaliwa kulingana na maelekezo yaliyotolewa katika mkutano wa nane wa namna hiyo uliofanyika Nairobi, Kenya, Desemba 11, mwaka jana, 2014.
 Mwenyekiti wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na mwenyeji wake Rais Paul Kagame wa Rwanda kabla ya kuanza kwa mkutano wa tisa wa wakuu wa nchi hizo kujadili miradi iliyoko katika Ukanda wa Kaskazini (Northern Corridor Integration Projects)  katika Hoteli ya Serena mjini Kigali.