Wednesday 26 January 2011


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM),Rais Jakaya Kikwete,akiendesha kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichofanyika juzi ambacho kiliendelea jana Ikulu jijini Dar es Salaam.
---
1. SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA CCM KUTIMIZA MIAKA 34

Kamati Kuu imejadili na kupitisha ratiba ya Sherehe za CCM kutimiza miaka 34 ambazo Kitaifa sherehe za Uzinduzi zitafanyika Mkoa wa Dar es Salaam tarehe 1/2/2011 na mgeni rasmi anatazamiwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar) Mhe. Aman A. Karume na kilele cha maadhimisho Kitaifa yatafanyika Dodoma ambako Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete atakuwa Mgeni rasmi. Kila Mkoa na Wilaya wataandaa ratiba zao kulingana na mazingira ya maeneo yao. Katika wiki hiyo ya sherehe wana CCM na wanachama wa Jumuiya za Chama watafanya mikutano ya hadhara kuwashukuru wananchi kwa kukipa ushindi Chama Cha Mapinduzi katika ngazi ya Urais wa Muungano, Urais wa Zanzibar, Ubunge, Uwakilishi na Madiwani.

Aidha sherehe hizi zitatumiwa kufanya mikutano ya Matawi na Kata kufanya tathmini kuhusu Uchaguzi uliopita na kuweka mikakati ya kujiandaa kwa Uchaguzi ujao.

Sherehe hizi pia zitaambatana na Matembezi ya Mshikamano yatakayofanywa nchi nzima asubuhi ya siku ya kilele, yaani tarehe 5/2/2011; haya ni matembezi yanayofanywa kila mwaka wakati wa sherehe hizi ili kudumisha umoja na mshikamano ndani ya chama na nchi kwa jumla; pia huwa ni fursa kwa wana CCM kuchangia Chama chao.


2. VURUGU KATIKA MANISPAA YA ARUSHA

Kamati Kuu imesikitishwa na tukio la vurugu za kisiasa zilizotokea tarehe 5 Januari, mwaka huu katika Manispaa ya Arusha ambapo watu watatu walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa pamoja na uharibifu mali. Kamati Kuu inawapa pole waliofiwa, waliojeruhiwa na wale ambao mali zao ziliharibiwa. Aidha ni matumaini ya Kamati Kuu kwamba tukio hili halitarudiwa tena hapa nchini kwani lengo letu sote ni kudumisha amani na usalama wa maisha ya wananchi na mali zao. Kuhusu maandamano yaliyozuiwa na Jeshi la Polisi lakini baadhi ya viongozi wa CHADEMA wakachochea yafanyike na hatimaye kusababisha wananchi kupoteza maisha yao, na wengine kujeruhiwa na uharibifu wa mali, kwa vile suala hili sasa lipo Mahakamani Kamati Kuu haitapenda kulizungumzia kwa undani. Imetoa angalizo kwa viongozi wa siasa wa vyama vyote kuwa wajibu wao wa kwanza ni kulinda amani na utulivu, na kujiepusha kabisa na uchochezi wenye kuleta chuki na ubabe wa kutunishana misuli na vyombo vya dola ambavyo ndiyo muhimili wa ulinzi na usalama wa nchi yetu na wananchi wote na mali zao.

3. UCHAGUZI WA MEYA MANISPAA YA ARUSHA
Kwa kuzingatia kwamba umekuwepo upotoshaji mkubwa kuhusu uchaguzi wa Meya wa Manispaa ya Arusha, na hata kusababisha malalamiko mengi na vurugu, Kamati Kuu inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao:-

Kwanza:
· Matokeo ya Udiwani Manispaa ya Arusha yalikuwa ifuatavyo: Madiwani wa Kata: CCM 10, CHADEMA 8 na TLP 1 – Jumla viti 19.
· Madiwani Viti Maalum: CCM 3, CHADEMA 3.
· Wabunge Viti Maalum: CCM 3, CHADEMA 3.

Matokeo ya jumla: CCM – Viti 16, CHADEMA 14 na TLP 1. Jumla Viti 31.

Pili:

Siku ya kupiga kura (tarehe 18/12/2010) Mkutano ulipoanza wajumbe 14 wa CHADEMA hawakuwepo. Waliofika ni wajumbe 16 wa CCM na 1 wa TLP, jumla wajumbe 17 ambao ni zaidi ya nusu ya wajumbe wanaotakiwa ili mkutano uwe halali kwa mujibu wa sheria.

Katika mazingira haya Msimamizi wa Uchaguzi aliendesha uchaguzi ambapo Ndugu Gaudence Vicent Lyimo wa CCM alipata kura 17, hivyo kutangazwa mshindi halali wa kiti cha Umeya na Ndugu Michael Kivuyo wa TLP alipata kura 17 na kutangazwa mshindi halali wa kiti cha Naibu Meya.

Kwa hiyo wanaosema uchaguzi huo haukuwa halali ama hawajui sheria au wanajiingiza tu katika ushabiki wa kisiasa.


Tatu:
CHADEMA wanadai katika wale wajumbe 16 wa CCM, mmoja wao (Mhe. Mary Chatanda) hakuwa mjumbe halali kwa kuwa katika kugombea Ubunge wa Viti Maalum aligombea kupitia Mkoa wa Tanga.

CHADEMA, kupitia Msimamizi wa Uchaguzi waliomba ufafanuzi wa kisheria kutoka Tume ya Uchaguzi, Katibu wa Bunge na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu. Ofisi zote hizo tatu zilitoa jibu kwamba Mhe. Mary Chatanda alikuwa mjumbe halali wa kikao hicho, na kwamba Wabunge Viti Maalum ni Wabunge wa Kitaifa na vyama vyao ndivyo vinawapangia Halmashauri za kufanyia kazi. Mhe. Mary Chatanda anaishi Arusha akifanyakazi kama Katibu wa CCM wa Mkoa huo hivyo CCM ilimpangia hapo hapo Arusha ndipo afanyie kazi za Halmashauri kama Diwani na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa iliarifiwa kuhusu uamuzi huu kama sheria inavyotaka.

Ni ufafanuzi huo huo ndio CHADEMA waliutumia kushinda kiti cha Halmashauri ya Hai baada ya kuwapangia kufanyakazi katika Halmashauri hiyo Wabunge 2 wa Viti Maalum na ambao si wakaazi wa Wilaya hiyo. Kura hizo mbili ndizo ziliwapa CHADEMA ushindi; na CCM tumekubali matokeo kwa kuwa kwa kufanya hivyo CHADEMA hawakuvunja sheria.

Uhalali wa Mhe. Mary Chatanda kupiga kura Manispaa ya Arusha ni sawa sawa na uhalali wa Wabunge wawili wa Viti Maalum wa CHADEMA walivyopiga kura Hai.

Jambo hili CHADEMA wanalijua vizuri lakini wanapotosha umma kwa makusudi wakitumia vyombo vya habari ambavyo bila kufanya utafiti navyo vimekuwa vinashabikia suala hili.

Kwa kifupi Kamati Kuu inasisitiza kwamba Uchaguzi wa Meya wa Arusha ulifuata sheria kwa ukamilifu, na washindi walishinda kihalali na hakuna sababu ya kurudia kufanya uchaguzi mwingine. Iwapo kuna watu hawaridhiki na mchakato wa uchaguzi huo wanayo nafasi ya kupinga katika vyombo vya sheria bila ya kufanya fujo wala kuleta uvunjifu wa amani kama ule uliotokea tarehe 5/1/2011 kule Arusha.

4. HUKUMU YA KUILIPA KAMPUNI YA DOWANS

Kamati Kuu imetafakari kwa makini suala la TANESCO kuilipa kampuni ya DOWANS Shs. 94 bn. na kubaini kuwa huu ni uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Biashara kwamba TANESCO ilivunja mkataba kinyume cha makubaliano na katika hali ya kawaida, kama hakuna njia nyingine ya kujiondoa kwenye kosa, ni busara na ni wajibu kwa muungwana kuheshimu maamuzi ya Mahakama. Hata hivyo, Kamati Kuu imeona kuwa kwa vile wapo Watanzania walioamua kupinga Mahakamani uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa wa TANESCO kuilipa DOWANS fidia ya Sh. bilioni 94, basi ni vema Serikali isubiri uamuzi wa Mahakama Kuu juu ya pingamizi hili.

5. MIGOMO NA MAANDAMANO VYUO VIKUU

Kamati Kuu imejadili hali inayojitokeza ya migomo ya wanavyuo na Wahadhiri katika vyuo mbali mbali kwa madai ya mikopo, na Wahadhiri kupunjwa mishahara. Kamati Kuu imeitaka Serikali ifuatilie kwa karibu sana madai ya Wanavyuo na Wahadhiri na yale matatizo ya dhati hatua za haraka zichukuliwe kuyapatia ufumbuzi ili wanavyuo na wakufunzi watumie muda wao madarasani na sio barabarani kwenye maandamano.

6. SEMINA YA WABUNGE WA CCM

Kwa kuzingatia maelekezo ya Kamati Kuu, CCM imeaandaa semina ya siku 3 ya Wabunge wake wote 260 itakayoanza tarehe 22 hadi 24/1/2011. Semina itafanyika Dar es Salaam katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, na itafunguliwa na Mhe. Mizengo Pinda (Mb.) - Waziri Mkuu na Mjumbe wa Kamati Kuu; na itafungwa na Mwenyekiti wa Chama Dkt. Jakaya M. Kikwete.

Mada kuu zitakazojadiliwa ni kuhusu Wajibu wa Ubunge na pia kuhusu Kanuni za Bunge. Kwa kuwa karibu asilimia 60% ya Wabunge wa CCM ni wapya, semina hii ina lengo la kuwapa uelewa mpana kuhusu majukumu yao ya Ubunge.

7. MKUTANO WA MAKATIBU WAKUU WA VYAMA VYA UKOMBOZI KUSINI MWA AFRIKA

Kamati Kuu ilipokea na kujadili taarifa ya Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Vyama vya Ukombozi Kusini mwa Afrika uliofanyika mjini Luanda, Angola tarehe 7-10 Desemba 2010 Vyama hivyo ni: ANC (Afrika Kusini), FRELIMO (Msumbiji), SWAPO (Namibia), MPLA (Angola), ZANU-PF (Zimbabwe) na CCM (Tanzania). Kamati Kuu imeyapokea mapendekezo yote yaliyotolewa na Makatibu hao ambayo baadaye yalijikita katika kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kimkakati wa vyama vilivyoongoza mapambano ya kudai uhuru katika nchi za Kusini mwa Afrika pamoja na uwepo wa haja ya kukusanya, kuratibu na kuhifadhi historia ya harakati za ukombozi ili kutunza vizuri urithi wa historia ya ukombozi kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Imetolewa na:-


Capt (Mst) John Z. Chiligati (Mb.),


KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA


ITIKADI NA UENEZI


21/01/2011