Leo
Tarehe 26 Novemba 2012, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Peter
Kallaghe amempokea na kumkaribisha Waziri wa Maji Mhe. Jumanne
Maghembe na ujumbe wake kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati
na Maji (EWURA) katika Ofisi za Ubalozi hapa nchini Uingereza.
Mheshimiwa Maghembe na ujumbe wake uko nchini Uingereza kwa ziara rasmi
ya kikazi na ya kiserikali. Ujumbe huo, ukiongozwa na Mhe. Maghembe,
utapata fursa ya kutembelea Makampuni, Taasisi mbalimbali za kiserikali
na binafsi zinazoshughulika na utoaji wa huduma ya Nishati na Maji hapa
Uingereza, vilevile Ujumbe huo utafanya
majadiliano na Viongozi Wakuu katika Sekta hiyo ya Nishati na Maji kwa
nia ya kupata ushauri wa Kitaalam wa kutafuta njia zaidi za kuboresha
utoaji wa huduma hizo nchini kwetu Tanzania.
Mheshimiwa Balozi Kallaghe, alitumia fursa hiyo kumfahamisha Mhe. Waziri Maghembe maendeleo ya kazi za Diplomasia ambazo Ubalozi unafanya kwa niaba ya serikali nchini Uingereza. Kwa upande wake Mheshimiwa Waziri Maghembe, alielezea mafanikio ya serikali katika kuwapatia wananchi huduma ya maji na juhudi zinazoendelea kufanywa kuondoa tatizo la Maji na kuhakikisha tatizo hilo linakuwa historia nchini Tanzania.
Waziri Maghembe anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo na viongozi wakuu wa sekta ya Nishati na Maji nchini Uingereza yenye lengo la . Aidha ujumbe huo wa Tanzania, ukiongozwa na Mheshimiwa Waziri Maghembe utamaliza ziara yake nchini Uingereza siku ya Alhamis, tarehe 29 Novemba 2012.