Sunday, 8 August 2010


Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha
--------


Na Juma Mohammed, Maelezo Zanzibar.
Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha amesema hajakata tama kisiasa kwani ikitokea fursa yengine yoyote ya kuwania Urais wa Zanzibar hatosita kugombea kwa kuwa anaamini anazo sifa zinazotakiwa na Chama cha Mapinduzi(CCM).


Nahodha ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Mwanakwerekwe alisema jana katika upandishaji bendera Tawi la CCM Mwanakwerekwe Mjini Unguja, alisema akiwa kijana anaamini nanaweza kutimiza matakwa ya CCM na wananchi wote kwa ujumla. “Napenda kuwaeleza kuwa mimi sijakata taamaa, bado nina matumaini na ikiwa itatokea fursa hiyo nitagombea tena, lakini kwa sasa ninayo kazi moja tu nayo ni kukisaidia Chama changu mgombea wetu Dk. Shein ashinde katika Uchaguzi Mkuu” Alisema Nahodha.


Waziri Kiongozi alisema kuwa kama walivyo wazee vijana nao wana uwezo mkubwa katika nafazi za uongozi na wanaosema vingine wamefilisika kisiasa. “Hata wazee wasiokuwa makini wapo kama ilivyo kwa baadhi ya vijana, lakini si sahihi vijana wakanyimwa nafasi ya uongozi eti tu sababu ya ujana wao” Alisema Nahodha ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 48.


Nahodha alitumia fursa hiyo kuwataka radhi waliokereka katika Jimbo lake juu ya hatua ya kuwania tena Uwakilishi akisema alifanya hivyo kwa faida ya Chama na Serikali na kuahidi ataweka uzito mkubwa kiutendaji katika Jimbo iwapo atawaa tena nafasi hiyo.
Akizungumzia umuhimu wa ujenzi wa majengo bora ya matawi ya CCM, Nahodha ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu, alisema majengo ya Chama hicho lazima yaendane na hadhi ya CCM.


Hata hivyo, alionya kwamba uhai na uimara wa CCM hautokani na majengo mazuri pekee, bali namna wanachama wake watakavyokienzi ndani ya nyoyo zao na viongozi kuwajibika. Nahodha alichangia ujenzi wa jengo hilo shilingi milioni 2 taslimu na kuahidi kutoa shilingi milioni tatu kabla ya Uchaguzi Mkuu ili kutoa msukumo kwa Tawi hilo liweze kutumika mapema.