Dar es salaam, Madereva wa boda boda
wakiongoza maandamano ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake jijini Dar es
salaam. Maandamano hayo yalianzia uwanja wa Tipi ulioko Sinza hadi katika hotel
ya Blue Pearl iliyopo Ubungo.
Dar es salaam, Ujumbe mbalimbali
wa maadhimisho ya kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Kilimanjaro, Maandamano yakipita
eneo la kituo kuu cha Mabasi cha mjini Moshi yakieekea katika viwanja vya kituo
hicho ambako uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia
kanda ya kaskazini
Kilimanjaro, Mkuu wa wilaya
ya Moshi, Novatus Makunga akisikiliza malezo kutoka katika banda la shirika la
NAFGEM linalopambana na vitendo vya Ukatili dhidi ya Wanawake.
Mwanza, Shirika la kutetea haki za
wanawake la KIVULINI la jijini Mwanza likikabidhi zawadi mbalimbali zikiwemo
laptop kwa waandishi walioandika habari zinazotetea haki za wanawake.
Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili
wa kijinsia inahitimishwa leo tarehe 10 Disemba ambayo ni siku ya kimataifa ya
tamko la Haki za Binadamu ikiwa ni ishara ya kuhusisha ukatili dhidi ya
wanawake na haki za binadamu na kutia msisitizo kwamba ukatili kama huu ni
ukiukwaji wa haki za binadamu.
Maadhimisho haya yalianza rasmi tarehe
25 Novemba siku ambayo ilichaguliwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1993 kuwa ni siku
ya kimataifa ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake ambapo kila mwaka, Umoja wa
Mataifa unashauri, mashirika ya Kimataifa na asasi zisizo za kiserikali kufanya
shughuli zinazolenga kufahamisha jamii juu ya ukatili wa kijinsia, hususani
ukatili dhidi ya wanawake.
Mwaka huu, kauli mbiu inasema FUNGUKA,
CHUKUA HATUA, MLINDE MTOTO APATE ELIMU yenye lengo la kuhamasisha jamii
kutambua changamoto mbalimbali zinazohatarisha usalama na kuchochea ukatili wa
kijinsia mashuleni ikiwa ni pamoja na suala la viboko kuendelea kuwa tatizo
kubwa, adhabu kali wanazopewa watoto ambao haiendani na umri wao pamoja na mila
na desturi potofu zinazokandamiza watoto wa kike kama mimba za utotoni na
ukeketaji.
Video: Uzinduzi wa siku 16 za
kupinga ukatili wa kijinsia: https://www.youtube.com/watch?v=TdGTQiAi4Fg
Mkurugenzi wa shirika la WiLDAF, Dr.
Judith Odunga akizungumza wakati wa ufunguzi wa kampeni hizi alitaja changamoto
nyingine kuwa ni miundombinu ambayo ni pamoja na kuwa na madarasa ya kutosha,
madawati, vyoo na sehemu za kujisitiri kwa watoto wa kike, mabweni, uzio
kuzunguka mashule pamoja na mazingira magumu ya usafiri wakati wa kwenda na
kurudi nyumbani na kutokuwa na chombo cha wanafunzi cha kutumika kusemea
matatizo yao pale ambapo wanakutana na changamoto mbalimbali.
Akiongezea, Dr. Odunga alisema kampeni
hii kwa mwaka huu ilifanyika kikanda chini ya uratibu wa mashirika na wadau
mbalimbali wa maendeleo. Kanda hizo ni kanda ya Ziwa (Mwanza, Mara na
Shinyanga), Kanda ya Kaskazini (Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga), Kanda
ya Kati (Dodoma, Morogoro na Singida), Kanda ya Kusini (Mtwara, Songea, Mbeya,
Iringa na Lindi), Kanda ya Pwani (Dar es salaam na Pwani) na kuratibiwa na
wadau mbalimbali wakiwemo mashirika ya KIVULINI, CWCA, NAFGEM, Morogoro
Paralegal, Mtwara paralegal, WiLDAF, TWCWC pamoja na Jeshi la Polisi.
Ujumbe wa maadhimisho haya na picha
zinapatikana kupitia ukurasa wa Facebook wa WILDAF ambao ni www.facebook.com/WILDAFTZ