JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA
|
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
MAABARA YA BRN KUCHAMBUA CHANGAMOTO YA MASOKO
KATIKA KILIMO
Jumatatu, April 21, April, 2015: Ofisi ya Rais-Ufuatiliaji wa
Utekelezaji wa Miradi (PDB) inayosimamia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN),
imealika wataalamu wa kilimo ili kuchambua na kutoa mapendekezo juu ya namna bora
nchi inavyoweza kutatua changamoto ya masoko kwa wakulima. Ili kufikia lengo
hilo, maabara ndogo ya siku tano imeandaliwa ili kutathmini mifumo ya sasa ya
masoko kwa mazao ya mahindi na mpunga.
Akifungua maabara hiyo jijini Dar
es Salaam, Jumatatu, Mtendaji Mkuu wa PDB, Bw. Omari Issa amewataka wadau wote
husika kufanya kazi hiyo kwa pamoja katika kuleta majibu yanayolenga mikakati
ya muda mfupi na mrefu ili kuwapatia nafuu wakulima.
Alisisitiza kuwa nidhamu ya
kiutendaji ya BRN inawataka wadau wa sekta za umma na binafsi kufanyakazi kwa
pamoja ili kutatua changamoto zinazozikabili sekta muhimu; ikiwemo ya kilimo na
kuongeza kuwa majibu ya changamoto za masoko kwa wakulima yatakoka kwenye pande
pande hizo mbili. Maabara hiyo ndogo inajumuisha wawakilishi 50 kutoka sekta za
umma, binafsi, taasisi za kimataifa na wakulima wenyewe.
Tanzania
nzima, na hususani miradi ya kipaumbele ya
kilimo iliyo chini ya BRN, ilishuhudia uzalishaji mkubwa wa mahindi na mpunga
katika msimu wa 2013/14; jambo ambalo limeleta fursa nzuri lakini pia lilikuja
na changamoto zake. Kwa mfano katika msimu huo, uzalishaji wa mahindi ulifikia
tani milioni 6 ikilinganishwa na uzalishaji wa tani milioni 4.5 kwa wastani katika
miaka mitano ya nyuma. Mpunga ulifikia tani milioni 1.7 kutoka tani milioni 0.85
mwaka uliotangulia.
Mwisho wa maabara hii, washiriki
wataibua mapendekezo na mpango wa utekelezaji utakaoainisha mfumo madhubuti wa
masoko ya mahindi na mpunga. Inatarajiwa kwamba mapendekezo haya yataweza
kutumika kwa mazao mengine pia.
Kwa maelezo zaidi, wasiliana na Mkurugenzi wa Mawasiliano na
Utetezi wa PDB:
Imetolewa
Dar es Salaam na:
Omari Issa, Mtendaji Mkuu,
Ofisi ya Rais-Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (PDB)
________________________
Kwa
wahariri:
Kuhusu
BRN
Mpango
wa Matokeo Makubwa Sasa! (BRN) ni: Mfumo maalum wa utekelezaji wa miradi
unaotumika kutekeleza Sekta Kuu za Kitaifa za Kipaumbele (NKRAs) kwa lengo la
kuharakisha upatikanaji wa huduma kwa umma ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa
ya Maendeleo, 2025, ya kuifanya Tanzania ifikie hadhi ya nchi yenye uchumi wa
kiwango cha kati. Mfumo wa BRN unajumuisha mkakati wa utekelezaji, muundo wa
usimamizi wa utekelezaji katika ngazi ya wizara na mipango mikakati. Kwa
pamoja, mikakati hii inajenga mfumo wa maendeleo unaoweka vipaumbele katika
ushirikishaji, uwazi na uwajibikaji.
Kuhusu Mfumo wa Maabara
Mfumo wa maabara katika BRN unahusisha kuwakusanya pamoja wataalamu na wadau wengine
husika ili kufanya uchambuzi wa kina na kupata suluhu ya changamoto, kuainisha
mikakati ya kipaumbele na kuainisha mpango wa kina wa utekelezaji wenye
viashiria vinavyopimika.