Monday 9 April 2012
















STEVEN KANUMBA -1984-2012





Mzalendo Mtanzania8 April 16:42
==========MAELEZO YA LULU NI HAYA=============
Baada ya kugoma kutoa maelezo kwa takribani siku nzima ya jana, mwanadada Lulu hatimaye amezungumza na polisi na kuelezea kilichotokea baina yake na marehemu Steven Kanumba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema Kanumba alikufa kutokana na ugomvi uliotokea kati yake na rafiki yake wa kike Lulu.

"Kanumba amefariki usiku wa kuamkia leo (jana) majira ya saa tisa usiku, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni ugomvi kati yake na rafiki yake wa kike anayejulikana kwa jina la Elizabeth Michael 'Lulu' mwenye umri wa miaka 18.

Alisema kabla ya ugomvi huo kutokea kati yao wakiwa chumbani, simu ya Lulu iliita na akaamua kutoka nje kupokea kitendo kilichomuudhi Kanumba.

Kamanda Kenyela alisema Kanumba aliamua kumfuata Lulu nje huku akifoka kwa sauti akitaka aelezwe kwanini alitoka nje kupokea simu huku akimtuhumu kuwa huenda alikuwa akizungumza na mwanaume mwingine.

Aliongeza baada ya Lulu kuona Kanumba akimfuata aliamua kukimbia kutoka nje ya geti , lakini kabla hajafanikiwa kufungua geti, Kanumba alimkamata na kumrudishwa ndani.

Kamanda Kenyela, alisema Kanumba akiwa amemshikilia waliingia wote chumbani na kufunga mlango.

Hata hivyo, alisema haijulikani nani aliyefunga mlango, ingawa maelezo ya Lulu anadi kuwa aliyefunga mlango ni Kanumba.

Kamanda huyo alisema Lulu anaeleza kuwa baada ya Kanumba kufunga mlango, alimuona akilegea na kujigonga kisogo chake kwenye ukuta wa chumba hicho kabla ya kuanguka chini.

Alibainisha kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa Kanumba alikuwa amekunywa Whisky (pombe kali) aina ya Jacky Daniel, hata hivyo, bado wanachunguza zaidi kujua kama kweli Kanumba alilegea tu na kuanguka, ama alipigwa na kitu kizito kichwani au alisukumwa kwa nguvu na kumfanya aangukie kisogo.

“Uchunguzi ukikamilika tutampeleka mahakamani kwa tuhuma za mauaji,” aliongeza Kamanda Kenyela.

Sambamba na jina lililotawala vinywani na akilini mwa watu wengi hivi leo, jina lingine ni la Elizabeth Michael au maarufu kama Lulu ambaye kama ilivyokuwa kwa Marehemu Steven Kanumba, naye pia ni muigizaji wa filamu nchini Tanzania(Bongo Movies).

Lulu anatajwa kuwa ndiye mtu ambaye mpaka dakika za mwisho alikuwa na Marehemu.Inaaminika kwamba wawili hao walikuwa wapenzi ingawa waliyafanya kwa siri kwani hivi karibuni wote wawili katika nyakati tofauti kupitia kipindi cha Mkasi kinachorushwa kila Jumatatu na East Africa Television, wote walikana kuwa na mahusiano na mtu yeyote.Walisema wapo Single.

Hivi sasa Lulu anashikiliwa na Polisi akiendelea kuhojiwa au kuwasaidia Polisi katika uchunguzi wanaoendelea kuufanya kufuatia kifo cha muigizaji huyo maarufu. Pamoja na kwamba vidole vingi kwa hivi sasa vinamuelekea binti huyu mdogo lakini ambaye mara kwa mara amekuwa akijaza kurasa za mbele za magazeti hususani yale “pendwa”,sisi hapa BC tunadhani ni busara zaidi kama tungeviachia vyombo vya dola(Polisi kwa wakati huu) kufanya uchunguzi wao wa kina kwanza.

Tunaamini kwamba Jeshi la Polisi litaweka hadharani taarifa kamili juu ya uchunguzi wao. Tuendelee kumuombea Steven Kanumba apumzike kwa Amani.Amina.