Wednesday, 4 November 2020

 



NAIBU Spika anayemaliza muda wake, Dk.Tulia Ackson akipokea fomu kutoka kwa Katibu Msaidizi wa Idara ya Oganaizesheni ya CCM, Solomoni Itundakwa aji ya kuomba kugombea unaibu spika wa Bunge. Tulia ni Mbunge Mteule wa Mbeya Mjini.


Dk Tulia akitoka  baada ya kuchukua fomu



Na Richard Mwaikenda, CCM Blog Dodoma.

NAIBU Spika anayemaliza muda wake, Dk.Tulia Ackson amesema ameaamua kugombea unaibu spika si uspika ili apate fursa ya kulitumikia vizuri jimbo la Mbeya Mjini.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuchukua fomu za kuwania tena nafasi hiyo katika Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), jijini Dodoma.

Amesema kugombea nafasi hiyo badala ya uspika si kwamba ameogopa ushindani utakaokuwepo kwenye nafasi hiyo ya juu, bali ameona unaibu spika unamfaa ili apate muda wa kuwatumikia vizuri wananchi wa jimbo la Mbeya.

alipoulizwa kwamba haoni kama kutogombea uspika anaogopa ushindani? Dk Tulia alijibu kuwa hadhani yeye kama ni mmoja wa watu wanaoogopa ushindani, kwa sababu hata jimbo alilogombea si jimbo la kawaida na kwamba yeye kama mdada ameweza kushinda hivyo kuwa mwanamke wa kwanza kuliongoza jimbo hilo.

"Hapana siyo kwa habari za ushindani,  Sidhani kama naogopa, kwanza mimi si mmoja wa watu wanaoogopa ushindani, kwa sababu jimbo ambalo nimekuwa mbunge si jimbo la kawaida  na mimi ni mdada ni wa kwanza kuliongoza. Nipo vizuri kwenye ushindani, lakini kwa sasa nimeona fursa hii naweza  kuliongoza jimbo na vilevile kumsaidia Spika endapo wawakilishi wa wananchi yaani wabunge wanatanipa ridhaa ya kutumikia nafasi hiyo", amesema Dk Tulia.


Dk. Tulia ambaye amehudumu kwenye unaibu spika kwa miaka mitano, amewaomba wabunge wampe tena ridhaa ya kushinda nafasi hiyo na kwamba yupo tayari kutumikia, kwani ana shauku ya kuona wabunge wanawawakilisha vizuri wananchi wao bungeni,

"Unaibu Spika ni nafasi ya utumishi, nipo tayari kutumika, miaka mitano iliyopita nilitumika naomba tena niendelee kutumikia kwani shauku yangu ni kuona wabunge  wakiwakilisha wananchi wao bungeni vizuri, kazi yao ni kuikumbusha serikali iliyoyaahidi iyatekeleze."