Thursday, 6 September 2012


Mjane wa Daudi Mwangosi aliyekuwa mwandishi wa Channel Ten,Itika akilia kwa uchungu juu ya kaburi la mumewe kwenye mazishi yaliyofanyika kijijini kwake Kasoka wilayani Rungwe mkoani Mbeya jana.Picha kwa hisani ya mbeyayetu.blogspot.com
KILA MMOJA AJITWISHA JUKUMU LA KUWASOMESHA, WAPIGANA VIJEMBE KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2015
Hawa Mathias, Mbeya na Tumaini Msowoya, Iringa
MAZISHI ya Mwandishi wa Habari, Daud Mwangosi yalifanyika jana katika Kijiji cha Busoka kilichoko wilayani Rungwe, Mbeya na kuhudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa. Katika mazishi hayo, viongozi hao wawili kila mmoja alitangaza kuwasomesha watoto wa marehemu Mwangosi ambaye alifariki dunia Septemba 2, mwaka huu baada ya kupigwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu wakati polisi walipokuwa wakisambaratisha mkutano wa Chadema.
Akitoa salamu zake katika mazishi hayo, Profesa Mwandosya alisema yupo tayari kumsomesha mtoto wa kwanza kati ya wanne wa Mwangosi, Nehemia ambaye anasoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Malangali.
Alisema atamsomesha mtoto huyo kidato cha tano na sita na ikiwa atafaulu na kukosa mkopo wa elimu ya juu, atamsomesha mpaka atakapomaliza elimu yake ya juu.
Dk Slaa kwa upande wake, alisema amewasiliana na rafiki yake ambaye yupo tayari kuwasomesha watoto wawili wa Mwangosi ambao wote wapo shule ya msingi. Mtoto wa mwisho wa marehemu hajaanza masomo.
Pamoja na kuwasomesha watoto hao, alisema Chadema kimetoa Sh2 milioni za rambirambi kutokana na msiba huo.
Vijembe msibani
Awali, Profesa Mwandosya na Dk Slaa walitoa kauli zinazoonyesha kupigana vijembe vya kisiasa, baada ya waziri huyo kumtaka Dk Slaa aache kufanya kampeni za kuingia Ikulu mwaka 2015 msibani.
Kauli hiyo ya Profesa Mwandosya ilikuja baada ya Dk Slaa kutaka polisi waliohusika na mauaji hayo wachukuliwe hatua za kisheria kwa sababu wanajulikana.
“Tunashangaa wamekamatwa watu wengine na kuwaacha waliohusika na mauaji hayo, tunawajua kwa sababu wameonekana hadharani, hakuna siri kwa hilo,” alisema Dk Slaa.
Akizungumza baada ya kauli hiyo ya Dk Slaa, Profesa Mwandosya aliwataka wanasiasa wa vyama vya upinzani kuacha kutumia misiba kutafuta kura za urais mwaka 2015.
“Natoa pole sana kwa familia na tasnia nzima ya habari nchini. Hiki ni kipindi kigumu, lakini tuviachie vyombo husika vifanye uchunguzi wa mauaji haya,” alisema Profesa Mwandosya na kuongeza:
“Lakini nichukue fursa hii kuwaomba wanasiasa waache kutumia misiba ili kujipatia umaarufu katika kutafuta kura za urais mwaka 2015.”
Katika mahubiri yake msibani hapo, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Busoka, Mathayo Mwanjemele alikemea mauaji hayo na kuwaomba wahusika wajitokeze hadharani kabla Mungu hajawaumbua.
“Waliohusika na mauaji haya wajitokeze na kutubu kwa wananchi kabla adhabu ya Mungu haijawakuta,” alisema.
Alisema ufike wakati Serikali iwe inakiri uzembe unaofanywa na watendaji wake ambao umekuwa ukitokea mara kadhaa.
IGP Mwema asimamia uchunguzi
Kabla ya mazishi hayo, mwili wa Mwangosi ulifanyiwa uchunguzi na wataalamu wa afya kutoka Dar es Salaam, huku IGP Said Mwema akishuhudia.
Baada ya kumalizika uchunguzi huo, usiku mwili wa marehemu ulisafirishwa kuelekea Mbeya kwa mazishi.
Mwili huo ulipofika Tukuyu, umati mkubwa ulijipanga barabarani na kupunga mkono, huku wengine wakiusindikiza kwa baiskeli na pikipiki hadi kijijini, Busoka.
Majeruhi wengine
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mafinga, Dk Peter Mwenda alisema mbali na marehemu Mwangosi, watu wengine 10 walijeruhiwa, wawili kati yao walitibiwa na kuruhusiwa. Alisema waliobaki hospitalini hapo hali zao zinaendelea vizuri.
Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Hussein Kweha (27), Edson Iddy (22), Alfred Kibitanyi (27), Hamad Musa (37), Yeremia Kulwa (45) na Christopher Pesa (30).
Alisema majeruhi hao walidai kwamba walikuwa katika mkutano wa ndani wa Chadema na askari waliwataka kutulia kabla ya kuwashambulia kwa marungu na vitu vyenye ncha kali.
Chanzo: mwananchi.co.tz