Sunday, July 1, 2012
HOTUBA YA MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANANCHI, TAREHE 30 JUNI, 2012
Kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa
Rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza nusu ya kwanza ya
mwaka 2012 salama. Kwa kutumia utaratibu wetu wa kuzungumza nanyi kila
mwisho wa mwezi, leo napenda kuzungumzia mambo mawili. Jambo la kwanza
ni suala la usafirishaji haramu wa binadamu nchini na la pili ni la
mgomo wa madaktari.
Usafirishaji Haramu wa Binadamu Nchini
Ndugu Wananchi;
Bila ya shaka mtakuwa mmezisikia taarifa za tukio la kushtusha na kuhuzunisha la kukutwa maiti 43
za watu wasiojulikana, zilizotupwa katika kichaka kilichopo kijiji cha
Chitego, Wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma tarehe 26 Juni, 2012. Pamoja
na maiti hao, walipatikana watu 84 wakiwa hai lakini wote wakiwa
wamedhoofu na baadhi yao wakiwa mahututi. Hatua za haraka zilichukuliwa
kuwasafirisha watu hao hadi Dodoma ambapo wale waliokuwa mahututi
walifikishwa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu na wengine
walihifadhiwa katika Kituo cha Kati cha Polisi, Dodoma. Maiti 22 zilipelekwa Dodoma na 21 zilipelekwa Morogoro kuhifadhiwa.
Taarifa
zilizopatikana kutoka kwa wale walionusurika zimebainisha kuwa watu hao
ni raia wa Ethiopia ambao walikuwa safarini kwenda Malawi na baadaye
Afrika ya Kusini ambako wangetengenezewa utaratibu wa kwenda kuishi
Marekani na Ulaya. Kwa mujibu wa maelezo yao, safari yao ilianza miezi
mitano iliyopita. Mwezi mmoja waliutumia Ethiopia na miezi minne
waliitumia Kenya kabla ya kuletwa Arusha ambako walipakiwa kwenye lori
na kuanza safari ya kuelekea Malawi lakini ikaishia Chitego. Lori
walilopanda lilikuwa limezibwa kabisa na hivyo kusababisha vifo kwa
kukosa hewa.
Tukio
la Chitego, Dodoma la wahamiaji haramu kukamatwa na wengine kukutwa
wamekufa si la kwanza kutokea hapa nchini. Kwa jumla, katika kipindi
cha takriban miaka 10 sasa kumekuwepo na tatizo kubwa la wahamiaji
haramu kuingia nchini. Kwa mfano, kati ya mwaka 2005 na hivi sasa jumla
ya wahamiaji haramu 19,683 wamekamatwa. Karibu wote wameshaondoshwa nchini na hivi sasa wapo karibu watu 1,500
tu magerezani wanaotumikia adhabu na kusubiri kurejeshwa makwao. Wengi
wa watu hao wanatoka Ethiopia na Somalia na baadhi kutoka Pakistan na
Bangladesh.
Wahamiaji
haramu wamekuwa wanaingia nchini kwa kupitia njia zisizo rasmi. Wapo
wanaotumia nchi kavu hasa kupitia mikoa ya Mara, Arusha, Kilimanjaro na
Tanga. Na, wapo wanaopitia baharini kwa kutumia fukwe za Pemba, Unguja
na za mikoa ya ukanda wa Pwani ya Tanzania Bara yaani Tanga, Pwani,
Lindi na Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Kwa
mujibu wa kauli zao, watu hao wamekuwa wanaeleza kuwa hawaji nchini
kuhamia bali wao ni wapita njia tu. Wanaelekea Afrika ya Kusini ambako
wameahidiwa kuwa watatengenezewa mipango ya kuhamia Marekani na Ulaya.
Watu hao pia wamethibitisha kuwepo kwa watu maalum wanaojihusisha na
usafiri wao tangu nchi watokako na zote wanazopitia mpaka kule
waendako. Aidha, wamesema kuwa wao wanawalipa watu hao ili
wawasafirishe na hakika si kiwango kidogo. Kwa jumla ni kwamba hili si
suala la uhamiaji haramu bali ni la biashara haramu ya kusafirisha
binadamu.
Ndugu Wananchi;
Kufuatia
vyombo vyetu vya usalama kuwa makini na watu wengi kukamatwa ndipo
wasafirishaji walipobuni njia za kuwasafirisha kama mizigo. Makontena,
malori yaliyofunikwa nyuma na matenki ya mafuta na ya maji yamekuwa
yanatumika kwa ajili hiyo. Usafiri wa aina hiyo ndiyo uliosababisha
vifo vilivyotokea Dodoma tarehe 26 Juni, 2012 na vya watu 21 vilivyotokea mwezi Desemba, 2011 Mkoani Morogoro, na vile vya watu 12 vilivyotokea katika matukio mawili ya Mkoa wa Mbeya, mwezi Mei, 2012.
Ndugu Wananchi;
Tarehe
27 Juni, 2012 nilikutana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama
nchini kuzungumzia tukio la Chitego na suala zima la biashara hii haramu
na hasa mbinu mpya inayotumiwa na wasafarishaji. Nilitoa pongezi kwa
vyombo vya dola kwa kazi nzuri waifanyayo kudhibiti shughuli za biashara
hii haramu hapa nchini. Tulielewana kuwa waendelee kuimarisha udhibiti
huo kwa lengo la kukomesha kabisa biashara hii.
Niliagiza
pia kwamba kikundi kazi nilichokiunda mwaka 2006 kushughulikia ujambazi
sasa kielekeze sehemu ya nguvu zake kukabili tatizo hili. Aidha, kwa
pamoja tulikubaliana kuwa nchi yetu ishirikiane na wenzetu wa Ethiopia,
Kenya, Malawi, Msumbiji na Afrika ya Kusini kutambua mawakala na
kuwabana kwa mujibu wa sheria. Tayari nimeshaanza kufanya mawasiliano
na baadhi ya Wakuu wa Nchi hizo kuhusu ushirikiano huo. Nashukuru wote
wameafiki nchi zetu zishirikiane kwa pamoja kuvunja mtandao huu mchafu
na kutokomeza biashara hii haramu na inayodhalilisha utu wa mwanadamu.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuchukua nafasi hii kuwashukuru wenzetu, wakazi wa vijiji vya Chitego
na Mkoka kwa kazi nzuri walioifanya. Kwa kweli, wenzetu wameonesha
uzalendo wa hali ya juu kwa kutoa taarifa mapema juu ya jambo lenyewe,
lakini pia wameonesha utu kwa kuwajali wageni waliokumbwa na janga hili.
Naushukuru pia uongozi wa Mkoa wa Dodoma na Morogoro ikiwa ni pamoja na
vyombo vya ulinzi na usalama kwa kulishughulikia tatizo hilo kwa
umakini mkubwa. Nimefurahishwa sana na ushirikiano ulioonyeshwa na
vyombo na taasisi mbalimbali za Serikali katika kushughulikia suala
hili.
Mgomo wa Madaktari
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ni kuhusu mgomo wa Madaktari unaoendelea nchini hivi
sasa. Nilipozungumza na Wazee wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Diamond
Jubilee tarehe 12 Machi, 2012, kuhusu mgomo wa Madaktari uliokuwa
unaendelea wakati ule pamoja na kuelezea chimbuko la mgomo na hatua
iliyokuwa imefikiwa, nilielezea mazungumzo yangu na viongozi wa Chama
cha Madakari wakiwemo pia viongozi wa Jumuiya ya Madaktari. Nilitoa
taarifa kuwa tumeelewana kuwa watasitisha mgomo na watarudi kwenye meza
ya majadiliano na Serikali. Siku ile pia nilielezea matumaini yangu
kuwa mgomo ule utakuwa wa mwisho katika nchi yetu. Bahati mbaya
matumaini yangu hayo hayakuwa na hivi sasa tunashuhudia tena wagonjwa
wakiteseka, kuhangaika na wengine kufa kwa sababu ya kukosa huduma
wanazostahili kwa vile madaktari wao wamegoma tena.
Ndugu Wananchi;
Kama
walivyoniahidi, madaktari waliacha kugoma na viongozi wao walirudi
kwenye mazungumzo na Serikali. Kama ilivyoagizwa na Mahakama Kuu,
Kitengo cha Kazi tarehe 8 Machi, 2012, kwa mujibu wa Sheria ya Mahusiano
Kazini, Namba 6 ya mwaka 2004. Chama cha Madaktari na Serikali
walifika katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (Commission for Mediation
and Arbitration) kwa ajili ya majadiliano. Kwa pamoja na kwa ridhaa yao
wote, pande hizo mbili ziliiomba Tume hiyo iwape fursa ya kuzungumza
wao wenyewe na wakimaliza mazungumzo wataenda kusajili makubaliano yao.
Tume ikawakubalia. Ni vizuri ikakumbukwa kuwa siku ile ya tarehe 8
Machi, 2012 Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, ilitoa zuio la mgomo pamoja
na kuagiza kuwepo mazungumzo baina ya pande mbili.
Ndugu Wananchi;
Kati
ya tarehe 10 Aprili, 2012 na tarehe 30 Mei, 2012, vilifanyika vikao
sita vya majadiliano kati ya Serikali na Chama cha Madaktari. Katika
mazungumzo hayo hoja au madai 12 ya madaktari yalizungumzwa. Mambo hayo
ni haya yafuatayo:
1. Posho ya kuitwa kazini (on call allowance) iwe asilimia 10 ya mshahara.
2. Posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi (Risk allowance) iwe asilimia 30 ya mshahara.
3. Madaktari wapatiwe nyumba grade A au posho ya makazi ambayo iwe asilimia 30 ya mshahara.
4. Posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu iwe asilimia 40 ya mshahara.
5. Madaktari walipwe posho ya usafiri ya asilimia 10 ya mshahara au wakopeshwe magari.
6. Madaktari wanaoanza kazi walipwe mshahara wa shilingi 3,500,00/= kwa mwezi.
7. Madaktari wapatiwe Green Card za Bima ya afya.
8. Hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
9. Viongozi wa Kisiasa kulazimisha kupewa rufaa nje.
10. Madaktari waliofukuzwa warudishwe kazini.
11. Huduma za afya ziboreshwe nchini.
12. Posho ya uchunguzi wa maiti iongezwe.
Ndugu Wananchi;
Katika mambo hayo 12 pande zote mbili zilifikia muafaka na kukubaliana wa pamoja kwa mambo saba. La kwanza,
ni kuhusu usafiri wa kwenda na kurudi kazini. Serikali ilieleza kuwa
upo utaratibu kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi wa Serikali Na. 3 wa
mwaka 2011 wa kuwakopesha wafanyakazi wa Serikali fedha za kununulia
magari au pikipiki, samani na matengenezo ya magari. Ilikubaliwa kuwa
madaktari waitumie fursa hiyo.
Jambo la pili,
ni kuhusu madaktari kupatiwa Green Card za Bima ya Afya. Jambo hili
lilikubaliwa na Serikali na Wizara ya Afya imekwishachukua hatua za
utekelezaji wake.
Jambo la tatu,
ni kuhusu hatua za kinidhamu kuchukuliwa dhidi ya Watendaji Wakuu wa
Wizara ya Afya. Kwa pamoja walikubaliana kuwa suala hilo liko nje ya
mamlaka ya Kamati yao ya pamoja, waziachie mamlaka husika za uteuzi.
Uongozi wa juu wa Wizara umebadilishwa na sasa kuna uongozi mpya.
Lakini, jambo la kustaajanisha hata Waziri mpya wa Afya alipowataka
waonane kuzungumzia hoja walikataa kumuona. Kwanza walisema hawaoni
sababu kwa vile wameyazungumza na Kamati yake kwa miezi mitatu bila ya
mafanikio
Jambo la nne walilokubaliana ni kuhusu viongozi kulazimisha kupewa rufaa ya kutibiwa nje. Walikubaliana mambo mawili. Kwanza,
kwamba maelekezo ya Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda kuwa madaktari
wazingatie maadili ya kazi zao na kukataa kutoa rufaa kwa mtu
asiyestahili awe kiongozi au asiwe kiongozi. Pili, walikubaliana
kuwa hospitali zilizopo ziboreshwe ili viongozi watibiwe hapa nchini.
Ukweli ni kwamba kufanya hivyo ndiyo sera ya Serikali. Nililieleza hili
mwezi Desemba 30, 2005 katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge baada ya
kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kuongoza nchi yetu.
Tumeiongeza sana bajeti ya sekta ya afya kutoka shilingi bilioni 300 2005/2006 hadi shilingi trilioni 1.2
mwaka 2011/12 na imekuwa ya tatu baada ya miundombinu na elimu.
Tumeziimarisha hospitali za Mikoa kwa vifaa tiba na wataalamu wa afya.
Kazi inaendelea katika hospitali za Wilaya. Tumewekeza katika Hospitali
ya Muhimbili. Hospitali hiyo ilivyo leo sivyo ilivyokuwa miaka sita
nyuma. Na kazi inaendelea hasa katika maeneo ambayo tunapeleka wagonjwa
nje. Matunda yake yanaanza kuonekana kwa upande wa figo, moyo, kinywa
na mipango inaendelea kwa upande wa ubongo na mishipa ya fahamu.
Tunaendelea kuimarisha mafunzo ya madaktari na madaktari bingwa, yote
kwa nia hiyo hiyo. Hivi sasa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba,Muhimbili
kinachukua wanafunzi wengi zaidi ya ilivyokuwa siku za nyuma na makazi
mapya ya chuo yanaendelea kuandaliwa ili kuchukua wanafunzi wengi zaid.
Mwaka 2005 tulikuwa na madaktari bingwa 46 mwaka huu tunao 520.
Ndugu Wananchi;
Jambo la tano ambalo pande zote mbili zilikubaliana ni kuhusu madaktari waliofukuzwa. Hawa ni wale Interns
waliokuwa wamerudishwa Wizarani kutoka Muhimbili na kupangiwa hospitali
za Temeke, Ilala, Mwananyamala na Lugalo. Hili ni jambo ambalo
lilikuwa limemalizika kitambo na wote walikuwa wamerudi Muhimbili.
Jambo la sita
ni kuhusu mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na madaktari kuhusu
kuboresha huduma ya afya. Mapendekezo hayo yalihusu kutathmini sera na
mpango wa afya ya msingi, bajeti ya afya kuwa asilimia 15 ya
bajeti ya Serikali, kuwepo na utaratibu mzuri wa kuajiri madaktari na
kuboresha viwango vya ubora wa madaktari na kadhalika. Serikali
imeyaafiki mapendekezo hayo na yatafanyiwa kazi.
Jambo la saba,
ambalo pande zote walilokubaliana ni kuhusu kuongeza posho ya uchunguzi
wa maiti. Hili ni jambo jipya halikuwepo mwazoni. Hata hivyo,
Serikali imelikubali na posho hiyo imeongezwa kutoka shilingi 10,000/=
hadi kufikia shilingi 100,000/= kwa daktari na shilingi 50,000/= kwa wasaidizi wake.
Ndugu Wananchi;
Kuna masuala matatu ambayo yamekuwa na muafaka kwa kiasi fulani na kutoafikiana kwa baadhi ya mambo. La kwanza
ni suala la kufanya kazi katika mazingira hatarishi. Serikali
imekubali hoja ya kuchukua hatua ya kuwalinda madaktari wanaofanya kazi
katika mazingira hatarishi. Serikali iliwaeleza kuwa watumishi wa kada
zote za afya watapatiwa chanjo dhidi ya maambukizi ya Hepatitis B na fedha zimetengwa katika bajeti ya 2012/13.
Aidha,
Serikali imeeleza dhamira ya kurudisha posho ya mazingira hatarishi kwa
watumishi wa umma wanaostahili. Utekelezaji wake utafanyika baada ya
uchambuzi wa kina wa kubainisha mazingira hatarishi ni yepi, viwango
stahiki viwe vipi na nani hasa wahusike. Madaktari wamekataa hili la
kufanya uchambuzi, wanataka kiwango kiwe kama wanavyotaka wao, yaani asilimia 30 ya mshahara na kianze mara moja.
Jambo la pili ambalo wamekubaliana nusu nusu ni kuhusu nyumba za
kuishi. Serikali imekiri wajibu wake wa kuwapatia madakari nyumba za
kuishi. Aidha, imeeleza mpango ulioanza wa kujenga nyumba 700 za madaktari kote nchini na kwamba hivi sasa ujenzi wa nyumba 90 unaendelea, 50 katika mkoa wa Mtwara na 40 katika mkoa wa Rukwa.
Kwa
maeneo ambayo madaktari wanalipwa posho ya pango Serikali imesema
waajiri wataendelea kufanya hivyo kwa mujibu wa taratibu zilizopo kwa
watumishi wa umma wenye stahili ya kupewa nyumba. Jambo hilo
limekataliwa na Madakari na kutaka lazima walipwe asilimia 30 ya
mshahara kama posho ya nyumba. Serikali kwa upande wake imeona vigumu
kufanya hivyo na kuwasihi wakubali wanayotendewa wafanyakazi wengine
wote wa umma.
Jambo lingine
ambalo lilikuwa na makubaliano ya nusu nusu ni kuhusu posho ya kufanya
kazi katika mazingira magumu. Pande zote mbili ziliafikiana kuwa yapo
baadhi ya maeneo nchini yanayo mazingira magumu kwa watumishi wa umma
hivyo hatua zichukuliwe kuwasaidia watumishi hao. Serikali imekubali
wajibu wa kuweka utaratibu wa kuboresha maisha ya watumishi katika
maeneo hayo. Kwa ajili hiyo, Serikali itatoa mwongozo kwa mamlaka za
ajira kuhusu namna ya kuwasaidia watumishi hao kupunguza makali ya
maisha katika kila eneo badala ya kutegemea posho peke yake.
Kuhusu posho, Serikali imeeleza kuafiki kuwepo posho ya aina hiyo ila
itatekelezwa baada ya kufanya uchambuzi wa kuainisha mazingira husika,
kutambua watumishi waliopo na gharama zake.
Madaktari hawajakubali kusubiri zoezi la uchambuzi lifanyike, wanataka
Serikali ilipe posho hiyo sasa. Tofauti hapa si posho hiyo kuwepo, bali
ni rai ya Serikali ya kubaini maeneo yenyewe na kupanga aina ya hatua
na viwango vya posho kulingana na mazingira halisi ya maeneo. Madaktari
hawaoni haja ya kufanya hayo.
Ndugu Wananchi;
Mambo mawili hayakuwa na muafaka kabisa kati ya pande zetu mbili.
Jambo la kwanza ni posho ya kuitwa kazini (on call allowance). Kwanza
sina budi kueleza kuwa Serikali imekubali kuongeza posho hiyo. Tangu
Februari, 2012 posho iliongezwa kutoka shilingi 10,000/= hadi shilingi 25,000/= kwa daktari bingwa (Specialist), shilingi 20,000/= kwa dakari mwenye usajili wa kudumu (Registrars) na shilingi 15,000/=
kwa madaktari waliohitimu ambao wapo katika kipindi cha mafunzo kazini
(Interns). Viwango hivyo vya posho vinatumika hivi sasa.
Madaktari kwa upande wao hawakukubali uamuzi huo wa Serikali na kusisitiza walipwe asilimia 10
ya mshahara. Ugumu wa kukubali pendekezo la madakari ni kuwa sharti la
malipo haya ni mtu kuitwa kazini. Ukitaka ilipwe kiwango cha mshahara
ina maana kuwa hata kama daktari hakupangwa kuitwa au alipangwa na
hakutokea aendelee kulipwa. Hili haliwezi kuwa sahihi kufanya.
Linaweza kuwafanya baadhi ya madaktari kutokutimiza wajibu wao kwa vile
wana hakika mwisho wa mwezi malipo yako pale pale.
Ndugu Wananchi;
Jambo
la pili ambalo muafaka haukufikiwa baina ya Serikali na madaktari ni
kuhusu mshahara wa kuanzia kazi wa daktari. Madaktari wanataka uwe shilingi 3,500,000/= wakati Serikali inasema kiasi hicho hatukiwezi. Serikali imeeleza utayari wake wa kuongeza mshahara kwa kati ya asilimia 15 mpaka 20
kama ambavyo itafanya kwa watumishi wote wa umma katika mwaka huu wa
fedha. Kwa kiwango cha sasa cha mshahara wao, daktari ataanzia kati ya shilingi 1,100,000/= na 1,200,000/= kutegemea kiwango kipi hatimaye kitaamuliwa. Madaktari wamekataa katakata na wameng’ang’ania shilingi 3,500,000/=.
Ndugu Wananchi;
Huo
ndiyo mlolongo wa mambo yaliyozungumzwa na pande zote mbili na matokeo
ya mazungumzo yenyewe. Katika kikao cha sita kilichofanyika tarehe 30
Mei, 2012, upande wa Chama cha Madaktari ulisema kuwa kwa vile hoja ya
nyongeza ya mshahara haina mabadiliko hawakuona haja ya kuendelea na
majadiliano mpaka watakapowasiliana na wenzao. Waliahidi kutoa taarifa
ndani ya wiki mbili. Tarehe 12 Juni, 2012, Rais wa MAT aliandika barua
kwa Katibu Mkuu Utumishi ambaye ndiye kiongozi wa majadiliano kwa upande
wa Serikali, kuwa Madaktari wameikataa taarifa na ufafanuzi waliopewa
kutoka Serikalini kwa ujumla wake.
Ndugu Wananchi;
Baada
ya majibu yale ya madaktari, tarehe 19 Juni, 2012, Serikali na
Madaktari walikwenda kwa Msuluhishi (CMA) kutoa taarifa kuwa mgogoro
umekosa usuluhishi kama sheria inavyotaka. Kwa pamoja pande zote mbili
zilikubaliana suala hilo lifikishwe Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi.
Wakati pande zote zinasuburi mgogoro huu kufikishwa ngazi hiyo ya juu,
upande wa Madaktari ukatangaza kuwepo kwa mgomo kuanzia saa sita ya
usiku tarehe 23 Juni, 2012. Hatua hiyo haikustahili kwani suala lenyewe
halijafika mwisho wa kushughulikiwa kwa mujibu wa Sheria za Mahusiano
ya Kazi nchini.
Ndugu Wananchi;
Tarehe
22 Juni, 2012, Mwanasheria Mkuu wa Serikali akaenda Mahakama Kuu
Kitengo cha Kazi kulifikisha suala la tishio la mgomo na kuomba zuio la
muda kufanywa. Mahakama Kuu ilikubali ombi hilo na kuagiza kuwa mgomo
usitishwe. Juhudi za kumtafuta Rais wa MAT, Dkt. Namala Mkopi na
viongozi wengine wa MAT hazikufanikiwa, Ofisi ya MAT ilikuwa imefungwa
na simu zote za viongozi wa MAT zilikuwa zimezimwa. Hatimaye tarehe 25
Juni, 2012, alipatikana na kupewa amri hiyo ya Mahakama. Tarehe 26
Juni, 2012, Dkt. Mkopi alifika Mahakamani ambapo alikana kuwa yeye
hahusiki na kuitisha huo mgomo lakini hakumtaja aliyehusika. Pamoja na
rai hiyo, Jaji alimuamuru Rais wa MAT akawatangazie wanachama wake
kusitisha mgomo. Dkt. Namala Mkopi hajafanya hivyo hadi leo na mgomo
umekuwa unaendelea kinyume cha Sheria.
Ndugu Wananchi;
Wagonjwa
wanateseka na wengine kupoteza maisha kwa mgomo huu usiokuwa halali
kisheria ambao pia haustahili kuwepo hata kwa mujibu wa maadili ya
udaktari. Viongozi wa MAT na wenzao wanawaingiza Madaktari katika
mgogoro na Mahakama na waajiri wao isivyostahili. Ni vyema viongozi wa
Madaktari na madaktari wakatambua kuwa wanashiriki katika mgomo usiokuwa
halali ambao pia kiongozi wao mkuu amekana Mahakamani kuwa hahusiki
nao. Madaktari lazima watambue pia kwamba ajira zao wanaziweka
hatarini. Mfanyakazi ana kinga ya kutofukuzwa kazi na mwajiri kwa
kushiriki mgomo unaokubalika kisheria. Huu siyo. Watapoteza ajira,
hawana pa kukimbilia, hawana cha kiwalinda. Kwa madaktari interns,
wanahatarisha maisha yao kwani hawatapata cheti cha kudumu wakishiriki
mgomo usiokuwa halali. Lazima watafakari sana kwa hayo wafanyayo.
Ndugu Wananchi;
Napenda kurudia maneno niliyoyasema tarehe 12 Machi, 2012, kuwa
kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi ni Sera ya Serikali yetu
kwa maelekezo ya Ilani ya Chama Tawala (CCM). Tumeitekeleza kwa vitendo
sera hiyo, hata hivyo ni ukweli ulio wazi kuwa nia yangu njema tu pekee
haitoshi, lazima uwezo wa kufanya hivyo uwepo. Kwa kulingana na uwezo
uliopo, tumeendelea kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi hatua
kwa hatua tangu tuingie madarakani. Tumefanya hivyo kwa jumla kwa
wafanyakazi wote na kwa kada mbalimbali za watumishi wa umma.
Miongoni
mwa wafanyakazi wa umma walionufaika na hatua hizo za Serikali ni
madaktari na watumishi wa kada nyingine za huduma ya afya. Tena
nadiriki kusema madaktari tumewapa upendeleo mkubwa kuliko watumishi
wengine wa umma. Upendeleo upo kwenye mafunzo ambapo wanafunzi wa
udaktari wanagharimiwa na Serikali kwa asilimia mia moja wakati
wanafunzi wenzao wa taaluma nyingine hawako hivyo.
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2004/2005, mshahara wa kuanzia wa daktari ulikuwa shilingi 178,700/=, mwaka 2005/ 2006 tuliupandisha na kuwa shilingi 403,120/=. Tuliendelea kuupandisha mwaka hadi mwaka mpaka kufikia shilingi 957,700/=
wanazolipwa sasa. Kiasi hicho ni mara mbili ya mishahara ya watumishi
wa taaluma nyingine wenye shahada ya kwanza wanaoanza kazi ambao kwa
wastani hupata shilingi 446,100/=.
Tunafanya
hivyo kwa kutambua na kuthamini nafasi maalum ya madaktari katika jamii
na ukweli kwamba bado tunayo safari ndefu ya kuziba pengo la madaktari
nchini. Lakini inaonekana juhudi zetu zote hizo hazithaminiwi.
Ndugu Wananchi;
Sina
budi kusisitiza kwamba tunapofanya hivyo tunaongozwa na uwezo tulio
nao wa kulipa. Kwa sasa hatuwezi kuwaahidi kuwa tunao uwezo wa
kuwalipa mshahara wa kuanzia wa shilingi 3,500,000/= na posho zote zile. Tukifanya hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi yatakuwa shilingi 7,700,000/=. Kwa hakika kiasi hicho hatutakiweza. Si vyema kutoa ahadi hewa kwa watu tunaowaheshimu na kuwathamini kama walivyo madaktari.
Kutokana
na ukweli huo basi kama daktari anayeona kuwa hawezi kufanya kazi
Serikalini bila ya kulipwa mshahara huo awe huru kuacha kazi na kwenda
kwa muajiri anayeweza kumlipa kiasi hicho. Nasi tutamtakia kila la
heri. Hana sababu ya kugoma ili ashinikize kulipwa mshahara huo.
Asisumbuke, hatalipwa mshahara huo. Isitoshe, hana sababu ya kuendelea
kuwa na mgogoro na mwajiri ambaye hana uwezo wa kumlipa anachokitaka.
Huna sababu ya kumpa usumbufu mwajiri wa kukuandikia barua ya kujieleza
au kukuachisha kazi. Kwa nini upate usumbufu wa kupata barua hizo na
kuzijibu. Kwa nini upate usumbufu wa kuachishwa kazi na kutakiwa
kuondoka kwenye nyumba ya Serikali ndani ya saa 24. Jiepushe na yote
hayo kwa kujiondoa mwenyewe. Usipofanya hivyo, mwajiri anakuwa hana
jinsi bali kukuondoa kazini maana unakwenda kinyume na sheria za kazi na
maadili ya kazi ya udaktari.
Mamlaka za ajira zimeanza kuchukua hatua hizo na wataendelea kufanya
hivyo kwa wote wanaoendelea kugoma. Najua baada ya hatua hizo
kuchukuliwa kuna manun’guniko ya kuonewa. Hivyo, mlitegemea mwajiri
afanyeje? Ni bora kufanya hivyo ili ajue hana daktari aweze kufanya
utaratibu wa kuziba hilo pengo na huyo ajae awe na mahali pa kuishi.
Vinginevyo atakuwa anajidanganya kuwa anae daktari ambae hayupo kazini
na wala hataki kufanya kazi.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuwathibitishia kwamba dhamira ya Serikali ya kuboresha maslahi ya
watumishi wa umma wakiwemo madaktari iko wazi. Tumekuwa tunafanya
hivyo, na tutaendelea kufanya hivyo kulingana na uwezo wa kibajeti. Ni
vyema watumishi wa umma wakatambua kuwa hatuwezi kutumia fedha zote au
kiasi kikubwa mno cha pesa za umma kulipana mishahara. Tukifanya hivyo,
Serikali itashindwa kutoa huduma muhimu kwa wananchi ambao ndiyo wengi
na wanastahili kuhudumiwa. Hata hizo huduma za afya tunazosema ni duni
tuziboreshe, hatutaweza kuziboresha kama tutatumia sehemu kubwa ya pesa
za Serikali kuwalipa mishahara wafanyakazi.
Hivi sasa matumizi ya mishahara ni asilimia 48 ya bajeti ya Serikali. Kiwango hicho ni kikubwa mno. Uwiano mzuri ni kuwa na matumizi ya mishahara yasiyozidi asilimia 35 ya bajeti na asilimia 65 zitumike kugharimia huduma na shughuli nyingine za maendeleo ya wananchi na taifa. Sisi tumezidi kwa asilimia 13. Hivyo, hatuna budi tukubali kujinyima kwa manufaa ya walio wengi.
Suala la Dkt. Steven Ulimboka
Ndugu Wananchi;
Kabla
ya kumaliza hotuba yangu, napenda kuungana na Watanzania wenzangu wote
kuelezea masikitiko yangu makubwa na kuhuzunishwa kwangu na kitendo cha
kinyama alichofanyiwa Dkt. Steven Ulimboka usiku wa tarehe 26 Juni,
2012. Kitendo hicho ni kinyume kabisa na mila na desturi zetu.
Watanzania hatujayazoea mambo hayo. Nimeelekeza vyombo vyetu vya ulinzi
na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane. Nimesema
kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la
kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa.
Natambua
kuwa Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka. Mimi
nimeshangazwa sana na hisia hizo kwani siioni sababu ya Serikali kufanya
hivyo. Dkt. Ulimboka alikuwa mmoja wa kiungo muhimu katika mazungumzo
baina ya Serikali na Madkatari. Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa
Serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano haya. Kulikuwa
na rai ya kutaka asiwepo, lakini nilisema wamuache maadam Madaktari
wanamuamini kuwa anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe
walioajiriwa na Serikali.
Ndugu Wananchi;
Kama
nilivyoeleza, mazungumzo yalienda vizuri na mafanikio makubwa
yamepatikana. Yapo maeneo machache na hasa eneo la mshahara ambalo
hatukuweza kukubaliana. Hapo tulipofikia si pabaya na tulikubaliana
sote kurudi kwenye mkondo wa Sheria kusaidiwa. Kwa nini Serikali
imdhuru Dkt. Ulimboka? Na, kuhusu mgomo, Mahakama Kuu imekwishatoa amri
ya kusitisha mgomo. Anayekaidi amri ya Mahakama ananunua ugomvi na
mhimili huo wa dola ambao wenyewe una mamlaka ya kumtia adabu mtu huyo.
Hivi baada ya kufika hapo Serikali iwe na ugomvi na Dkt. Steven
Ulimboka kwa sababu ipi na jambo lipi hata iamue kumdhuru? Kama kuna
mtu wa Serikali kafanya, itakuwa kwa sababu zake binafsi na siyo za
Serikali au kwa kutumwa na Serikali.
Ndugu Wananchi;
Kwa
niaba yangu na kwa niaba ya Serikali natoa mkono wa pole kwa Dkt.
Steven Ulimboka na kumuombea apone haraka ili aungane na familia yake na
Watanzania wenzake katika ujenzi wa taifa. Kwa namna ya pekee
namshukuru na kumpongeza Bwana Juma Mgaza, kwa moyo wake wa huruma na
upendo na kwa hatua alizochukua za kumsaidia Dkt. Ulimboka.
Naomba
kumaliza kwa kuwasihi madaktari kuacha mgomo na kurejea kazini.
Watanzania wenzenu wanateseka na kupoteza maisha. Muwe na moyo wa
huruma na upendo na msaada kwa wagonjwa kama kiapo chenu kinavyowataka.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.
P