SIMANZI na vilio jana vilitawala kwenye mazishi ya watu 2O waliofariki dunia kwa kufunikwa na kifusi kilichoporomoka mlimani na kufukia nyumba zao usiku wa manane katika Kata ya Mamba Miamba,wilayani Same,Kilimajaro.Gazeti la Mwananchi lilishuhudia watu zaidi ya 1,000 waliokusanyika katika msiba huo mkubwa wakiwa wamefunikwa na simazi,huku wakilia kwa uchungu kutokana na kupoteza ndugu zao katika mkasa huo wa kutisha.Asilimia kubwa ya watu walionyesha masikitiko yao,hasa kwa familia ambayo imepoteza watu 15 na kati ya hao wanne hawajapatikana mpaka sasa.Wanachi hao waliiomba serikali iwasaidie kutafuta miili ya watu hao na ikiwezekana watumie kikosi cha mbwa ili kubaini mahali ilipo.Elineema Shambi,mmoja wa ndugu wa wanafamilia 15 waliofariki dunia na ambaye alinusurika kwa vile alikuwa amekwenda mjini Moshi kwa shughuli za kibiashara,alisema kwa majonzi kwamba amepoteza mke na watoto wake wanne ambao walifukiwa na kifusi hicho.Alisema alikwenda mjini Moshi kununua bidhaa za kuuza,na kesho yake asubuhi alipigiwa simu na kuondoka mara moja. Alieleza kuwa alipofika alikuta nyumba yake imefunikwa kabisa kiasi cha kutoonyesha kama kulikuwa na nyumba na mwili wa mkewe ulikuwa haujapatikana hivyo akasaidia kuutafuta na kuupata pamoja na miili ya watoto wake.Alifahamisha kuwa yeye ni mmoja kati ya ndugu wa watu 15 waliofariki katika tukio hilo la kutisha.Akisimulia juu ya maporomoko hayo,alisema,dalili za mlima huo kuporomoka zilianza kuoneka mwaka jana kwa kuwa kulikuwa na ufa,hata hivyo hakueleza kwamba ni kwa nini hawakuhama katika eneo.Akiunga mkono maelezo hayo,Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,Monica Mbega alibainisha kuwa wananchi wa Kata ya Mamba Miamba walishaona dalili za kuporomoka kwa mlima ulioua watu 20,tangu mwaka jana,lakini hawakuchukua tahadhari.